1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika Kusini wataka kun'golewa kwa Zuma

1 Desemba 2013

Maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini Jumamosi (30.11.2013) wametowa wito kupitia mtandao wa kushtakiwa kwa Rais Jacob Zuma baada ya kufichuka kutumika fedha za serikali kuifanya nyumba yake binafsi iwe ya kifahari zaidi.

https://p.dw.com/p/1AR4F
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.Picha: picture-alliance/dpa

Magazeti ya kila wiki ya Mail na Guardian yamesema hapo Ijumaa kwamba repoti ya awali iliotolewa na taasisi ya kupiga vita rushwa nchini Arika Kusini imegunduwa kwamba Zuma amenufaika sana kibinafsi kutokana na mpango wa kuimarisha usalama nyumbani kwake uliogharimu dola milioni 21 ukijumisha bwawa la kuogelea na boma la kufugia n'gombe.

Waraka huo uliovuja wa Mwanasheria wa serikali Thuli Madonsela uliopewa jina "Ukwasi wa Kiwango cha Juu" umependekeza Zuma alipie baadhi ya fedha hizo za umma zilizotumika kuboresha eneo la nyumba yake ilioko huko Nkanda katika milima ya jimbo la KwaZulu Natal.

Repoti hiyo ya uchunguzi uliofanywa na Madonsela imechemsha ghadhabu kwenye mtandao wa jamii ambapo mwanaharakati mashuhuri Zackie Achmal ameanzisha ombi la kusainiwa kwenye mtandao la kutaka kun'golewa kwa Zuma ambalo limepata wafuasi 8,200 ikiwa ni saa 24 na ushee baada ya kuibuka kwa habari hizo. Repoti hiyo yumkini ikaimarisha dhana ya kutopea kwa rushwa chini ya utawala wa Zuma na inaweza kumharibia yeye pamoja na chama chake cha ANC katika uchaguzi uliopangwa kufanyika baada ya kipindi cha miezi sita.

Zuma ashtakiwe

Mfuasi mmoja aliechangia katika ombi hilo la mtandao Yoliswa Dwane ameandika mamilioni ya fedha za umma yametumika kuinufaisha nyumba binafsi ya rais wakati mamilioni ya watu hawana huduma muhimu kama vile maji,umeme na elimu ya kuheshimika.Amesema " Hii ni rushwa na ni tusi kwa maskini na wananchi wote wa nchi hii."Magazeti ya Afrika Kusini pia yameongezea sauti yao ambapo gazeti la Citizen likiwa na kichwa cha habari kwenye ukarasa wake wa mbele kinachosema "Mshtakini Zuma".

Wananchi wa Afrika Kusini katika kitongoji duni cha Soweto.
Wananchi wa Afrika Kusini katika kitongoji duni cha Soweto.Picha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

Msemaji wa Zuma amekataa kuzungumzia repoti hiyo wakati ofisi ya Madonsela imesema kuvuja kwa repoti hiyo "sio uadilifu na kinyume na sheria".Chama tawala cha ANC kimesema kinaamini kwamba Zuma hakutenda kosa lolote.

Zuma akosolewa

Magazeti ya Mail na Guardian yamesema kuboreshwa kwa eneo la nyumba yake hiyo kunajumisha sebule ya wageni ukumbi wa sinema,boma la kufugia n'gombe na bwawa la kuogelea ambalo katika waraka huo limetajwa kama bwawa la moto lilioko uwanjani ambalo linaweza kuongezea maradufu akiba ya maji kwa ajili ya kuzima moto.

Kwa mujibu wa magazeti hayo repoti hiyo ya Madonsela imemkosowa Zuma mwenye wake wengi,mfuasi mkubwa wa mila za kabila lake la Zulu ambaye kipindi chake cha miaka mitano madarakani kimezongwa na kashfa kutokana na kukiukwa kwa maadili kwa kushindwa kulinda rasilmali za taifa na kulipotosha bunge.

Zuma aliliambia bunge mwaka jana kwamba majengo yote yaliokuweko kwenye eneo lake hilo kubwa yamejengwa na wao wenyewe wakiwa kama familia na sio na serikali.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Bruce Amani