1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

African Diaspora

Kabogo Grace Patricia20 Novemba 2009

Inaaminika kuwa Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo wanaweza kuchangia maendeleo na kufikiwa kwa malengo ya milenia mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/Kc2S
Mmoja wa wahamiaji akiwa katika bandari ya Los Cristianos, Hispania.Picha: AP

Miongo kadhaa iliyopita Waafrika wengi wamekuwa wakiondoka katika bara hilo kutokana na sababu za kisiasa, kiuchumi au kijamii. Wengi wao wanaoondoka wanaaminika kuwa ni wataalam hivyo kuhatarisha mfumo mzima wa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa katika nchi wanazotoka. Wakati idadi ya Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo ikiongezeka, umuhimu kwa wao kuwa sehemu ya maendeleo katika bara hilo, unaongezeka kwa kuwa Afrika inahitaji zaidi wataalamu wenye ujuzi mkubwa, ili kufikia malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015. Karimi Kilemi-Kuhn anayetokea Kenya amekuwa akiishi na kufanya kazi nchini Ujerumani tangu mwaka mmoja uliopita na anaamini kuwa Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo wanaweza kuchangia maendeleo zaidi ya bara hilo. ''Badala ya kuwaacha wahisani wote hawa walete miradi yao Afrika, sisi kama Waafrika pia tunaweza kujiandaa kama kundi moja na kuanzisha miradi yetu ambayo inaweza kuchangia maendeleo katika bara letu. Kwa sababu bara la Afrika hata kama tutaendelea kuishi nje ya bara hilo, bado linabakia kuwa bara letu tu,'' alisema Karimi.

Wataalamu mbalimbali wanasemaje?

Wataalamu wanaamini kuwa Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo wanaweza kuanzisha uhusiano wa kibiashara katika nchi wanazotoka, kutoa msaada wa wataalam katika nyanja mbalimbali au kuanzisha miradi yenye lengo la kuleta maendeleo katika sekta muhimu kwenye jamii. Tayari kuna miradi ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kulisadia bara la Afrika. Mfano wa miradi hiyo ni ule unaowapeleka wataalamu mbalimbali kwenye nchi zao kwa kipindi kifupi kwa ajili ya kutoa msaada wa kiufundi. Mradi huu ulianzishwa mwaka 2001 na shirika lisilo la kiserikali la Migration for Development in Afrika, ambapo msemaji wake Chauzy Jean-Phillipe anasema, ''Uhamaji na wahamiaji siyo sehemu ya mipango yote ya kupunguza umasikini au siyo sehemu ya mpango wa kujaribu kufikia baadhi ya malengo ya maendeleo ya milenia. Hivyo, jukumu letu kama shirika la kiserikali ni kuhakikisha kuwa wahamiaji na uhamaji sasa ni sehemu ya kusawazisha maendeleo. ''

Serikali husika zinapaswa pia kuwajibika

Lakini mashirika ya maendeleo siyo tu wenye kuhimiza wahamiaji kuchangia kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao, serikali za nchi hizo pia zina jukumu lake katika kuhakikisha maendeleo katika nchi husika yanapatikana. Hivi karibuni nchi nyingi za Afrika zimeona umuhimu kwa wananchi wake waliopo nje kuwa sehemu ya kufikiwa kwa malengo. Katika nchi hizo zimeanzishwa wizara mpya zinazoshughulikia masuala ya wananchi wao waliopo nje. Waafrika wanaoishi nje ya bara hilo hawatachangia tu maendeleo katika bara hilo, bali pia kufikiwa kwa malengo ya milenia mwaka 2015.

Mwandishi: Sarah Bomkapre Kamara (Afrika/Nahost)

Imetafsiriwa na: Grace Patricia Kabogo

Mhariri: Abdul-Rahman