1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waalgeria wapiga kura leo katika uchaguzi wa Rais.

9 Aprili 2009

Bouteflika atarajiwa kuendelea kwa mhula watatu.

https://p.dw.com/p/HTQP
Rais Abdelaziz Bouteflika,Picha: AP

Waalgeria wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais , huku rais aliye madarakani Abdelaziz Bouteflika akitarajia kuutumia mhula wa tatu wa madaraka yake kumaliza machafuko yanayoendelea kulisibu taifa hilo lenye utajiri wa mafuta. Lakini kweli ataweza kufanya hivyo bila ya kuwapa sauti ya kisiasa waasi wa zamani ?

Rais Bouteflika anatarajiwa kushinda uchaguzi huo kwa wingi mkubwa kwa sababu ya kutokuwepo kwa mpinzani madhubuti na kutokana na mchango wake hadi sasa katika kuleta hali ya utulivu baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ya muongo mmoja.

Baadhi ya waasi wa zamani sasa wana mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na hufanya hujuma za mara kwa mara nchini Algeria yenye wakaazi milioni 34 na mwanachama wa umoja wa nchi zinazoasafirisha mafuta kwa wingi OPEC iko karibu sana na Umoja wa Ulaya

Acht Tote bei Selbstmordanschlag in Algerien
Uharibifu baada ya mripuko katika kituo cha polisi cha Zemmouri el Bahri, moja wapo ya mashambulioi ya waasi.Picha: picture-alliance/ dpa

Baadhi ya wadadisi wanaamini kwamba kukataa kwa Rais Bouteflika kuwaruhusu baadhi ya viongozi wa chama cha kiislamu FIS kilichovunjwa na ambacho kilipigana na dola miaka ya 1990 kubatilishwa uchaguzi ambao kikikaribia kushinda 1992, kunahujumu juhudi za kuwashawishi waasi waliobakia ambao wengi ni vijana, kuweka chini silaha zao.Watu 150.000 waliuwawa katika mapigano na umwagaji damu wakati wa mgogoro huo.

Viongozi hao wa zamani wa waasi wamelaani matumizi ya nguvu na kupewa msamaha, chini ya mpango wa maridhiano na upatanishi wa taifa wa Bouteflika mwenye umri wa miaka 72.

Msamaha huo unawapa haki za kiraia waasi wa zamani na kuzilipa fidia familia zao na baadhi yao wameingia katika biashara na kufanikiwa.

Lakini msamaha huo haukufafanua iwapo waataruhusiwa kurudi tena katika siasa. Hakuna sheria inayowazuwia viongozi wa zamani wa waasi kushiriki katika uchaguzi, lakini katika kipindi cha miaka kadhaa, juhudi za baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha zamani cha FIS kutaka kuwa wagombea au kuunda vyama zimezuiwa na serikali.

Viongozi wanne wa zamani waliwataka waasi waliosalia kujisalimisha wakisema " Awali tulikua ni wenzenu na nyoyo zetu ziko pamoja nanyi. Lakini tunawaomba mjiunge nasi na kurudi katika familia zenu zinazowasubiri."

Kikwazo ni kuwa Bouteflika haonekani kuwa na nia ya kutoa ridhaa ya aina yoyote kwa waasi siku za usoni. Wakati majeshi ya usalama yanaidhibiti vyema hali ya mambo hivi sasa kuliko miaka ya nyuma na ikiwa Bouteflika atachaguliwa tena kwa mhula wa tatu, hakuna shinikizo kubwa linaloweza kumkabili . Hivi karibuni aliwaambia mamia ya wafuasi wake mjini Tiaret kwamba waasi wa zamani waache kulalamika, badala yake wawaombe msamaha raia kwa maovu waliofanya.

Wachambuzi lakini wanasema kuwaruhusu waasi wa zamani wajiunge tena na siasa itakua hatua muhimu ya ziada kwani ni swala hilo hasa lililozusha mgogoro uliotokea.

Muasisi wa kundi lilovunjwa la Islamic Jihad-GIA- Abdelhaka Layada , ambalo linalaumiwa na maafisa wa serikali kwa wimbi la mauaji mnamo miaka ya 1990, anasema wanamuunga mkono Bouteflika, lakini badala yake wanataka kurudi katika maisha ya harakati za kawaida za kisiasa-kuwafungia uwanja huo si haki na pia ni hatari.

Kwa jumla yaelekea hali ya usalama nchini Algeria imefungamana na uhuru wa kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa waalgeria wote bila ya kipingamizi.