1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 9 wauwawa Myanmar.

Sekione Kitojo27 Septemba 2007

Waandamanaji wameingia tena katika mitaa ya kati ya mji mkuu Rangoon leo Alhamis, bila kujali ripoti za majeshi ya usalama kuwauwa watawa kadha pamoja na raia mmoja wa Japan , wakati majenerali wa Burma wakijaribu kuzima vuguvugu kubwa kabisa la kupinga utawala wa kijeshi kuwahi kuonekana karibu miaka 20 iliyopita.

https://p.dw.com/p/CB0u
Watawa wa dini ya Kibudha wakiwa katika maandamano mjini rangoon.
Watawa wa dini ya Kibudha wakiwa katika maandamano mjini rangoon.Picha: AP

Watu walijikusanya kuwazunguka watawa wanne waliokuwa wamesimama katikati ya barabara inayoelekea Sule Pagoda , eneo linaloishia maandamano wiki hii ambayo hivi sasa imefungwa.

Zaidi ya watu 1,000 waliwazunguka watawa hao wakati polisi wa kuzuwia ghasia wakiangalia wakiwa wameshika ngao zao, watu walioshuhudia wamesema.

Hajafahamika mara moja ni watawa wangapi ambao wamekuwa wakiongoza maandamano hayo watajitokeza ama ni kiasi gani cha watu wa kawaida ambao watathibutu kufanya maandamano baada ya msako uliofanywa mapema asubuhi ya leo dhidi ya majumba ya watawa wanaoonekana kuwa ni waasi.

Wakipuuzia miito kadha ya kimataifa ya kujizuwia na kuwa na uvumilivu , majenerali wa utawala wa Rangoon waliamuru vikosi kuingia katika majumba ya watawa mjini Rangoon na kwingineko na kuwakamata mamia kadha ya watawa.Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Chiristopher Hill amesema wakati akiwa katika ziara nchini China leo , kuwa utawala wa kijeshi wa Burma unapaswa kufahamu kuwa mzozo uliopo sasa haupaswi kutatuliwa kwa matumizi ya nguvu, bali unahitaji maridhiano.

Lakini hali ya wasi wasi imetanda kwamba inaweza kurejewa hali iliyotokea mwaka 1988, wakati majeshi yalipowauwa kiasi cha watu 3,000 katika ukandamizaji mbaya kabisa wa vuguvugu la uamsho lililotokea nchi nzima. Wakati majeshi ya usalama yameweka uzio wa waya katika makutano muhimu ya barabara katikati ya mji wa Rangoon , watawa wakiwa katika radio zinazozungumza lugha ya Kiburma nchi za nje wamewataka wenzao kutosalim amri.

Wanajeshi walifyatua risasi dhidi ya kundi la waandamanaji leo Alhamis wakati mamia kwa maelfu ya waandamanaji wanaodai demokrasia nchini Burma walionyesha ujasiri kwa kupuuzia msako mkubwa uliofanywa na majeshi ya nchi hiyo na ambao umesababisha miito ya kimataifa ikitaka utawala huo kuwa na uvumilivu.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice , ambaye leo Alhamis amewataka mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya Asia kujadiliana kuhusu hali katika nchini mwanachama Burma, ameutaka utawala huo kumruhusu mwakilishi maalum wa umoja wa mataifa kufanya mazungumzo na upande wa upinzani pamoja na kiongozi aliyewekwa chini ya ulinzi nyumbani kwake Aung San Suu Kyi.

China imesema hadharani pia kwa mara ya kwanza leo , kuwa utawala wa Burma unapaswa kujizuwia na matumizi ya nguvu. Matamshi hayo yanafuatia mkutano kati ya mwakilishi wa ngazi ya juu wa Marekani , ambaye ameitaka China kutumia ushawishi wake kama nchi jirani na mshirika wa kibiashara wa utawala huo wa kijeshi. China ikiwa moja kati ya washirika wachache wa utawala huo wa kijeshi inaonekana kuwa ina ushawishi mkubwa.