1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali tete nchinii Iran

22 Juni 2009

Nchini Iran baada ya siku mbili za machafuko, licha ya onyo Kali kutoka kwa kiongozi wa ngazi za juu nchini Iran, nchi hiyo sasa inasema inajua nani wa kulaumiwa, akiyanyooshea kidole mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/IWNi
Polisi wa kupambana na ghasia mjini TeheranPicha: AP

Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Iran ilisema mataifa ya Magharibi na vyombo vya habari vya magharibi vilichochea uharibifu na vurugu nchini humo, na hilo halikubaliki. Kituo cha redio cha taifa, nacho kiliripoti kuwa watu 457 wametiwa nguvuni, baada ya machafuko ya Jumamosi mjini Tehran yaliyosababisha vifo vya watu 10. Haya yote yanajiri huku mgombea aliyeshindwa Mir Hossein Mousavi akiwataka wafuasi wake waendele kukaza kamba ya upinzani.


Kulingana redio ya taifa ya Iran, kwa mara ya kwanza tangu upinzani kuibuka dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Juni 12- mji wa Tehran ulikuwa tulivu usiku kucha.

Iran Wahlen Samstag Demonstration Unruhen in Teheran
Mwanamke moja aliyejihami kwa jiwePicha: AP

Mnamo siku ya Jumamosi mji huo mkuu ulishuhudia machafuko mabaya kabisa tangu upinzani walipopeleka kilio chao barabarani kudai matokeo ya kura yalikuwa na udanganfifu. Watu 10 wanaripotiwa kuuawa katika makabiliano kati ya polisi wa kupamabana na vurugu na waandamanaji.

Na sasa serikali ya Iran inasema inajua nani wa kulaumiwa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Manoucher Mottaki jana aliliambia jukwaa la wanadiplomasia mjini Tehran kwamba Iran imechukizwa na jinsi Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zinavyotaka kuingiza kidole chake katika maslahi ya ndani ya Iran. Viongozi wa nchi hizi tatu wamekuwa mstari wa mbele kutilia shaka matokeo ya Iran na kuutolea wito wa utawala wa Iran kuwapa haki yao ya kismingi waandamanaji kukusanyika na kusema mawazo yao. Na leo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni, Hassan Qashqavi alitilia mkazo swala hili, akisema uchochezi wa nchi za magharibi na vyombo vya habari vya kimagharibi katika vurugu na machafuko nchini Iran ni jambo halitokubaliwa,'' Nimetoka katika mkutano na baraza kuu la kisheria, ambao pia ulihudhuriwa na kamati ya mambo ya kigeni ya bunge, tumezungumzia jinsi mataifa ya magharibi yalivyoingilia uchaguzi huu kabla , wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi. Tumepata ushahidi kuwa wa kuhusika kwa vitengo vya upelelezi, vya kisiasa na vyombo vya habari vya nchi za nje na sasa tumewasilisha ushahidi huo bungeni''


Nchi za Magharibi lakini hazijasita kuzungumzia Iran- Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kuhesabiwa upya kwa kura nchini Iran, na kuutaka utawala wa nchi hiyo kuheshimu haki za kibinadamu za raia wake,'' Nadhani mtu anaweza kuwa na shaka zaidi. Na kwamba uchaguzi ukirudiwa kuwe na uwazi zaidi, pamoja na waangalizi wa kimataifa, na hapo ndio imani inaweza kurudi. Na nalichukulia hili kama hatua ya kwanza kuweza kufanikisha hali bora zaidi.''alisisitiza.



Iran Wahlen Ali Akbar Hashemi Rafsandschani
Rais wa zamani wa Iran Ali Akbar Hashemi RafsanjaniPicha: AP

Na leo redio ya taifa imeripoti kwamba watu 457 wametiwa mbaroni kufuatia machafuko hayo ya siku ya Jumamosi. Jamaa watano wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ali Akbar Hashemi Rafsanjani walikuwa miongoni mwa wale waliotiwa mbaroni. Wote lakini akiwemo mtoto wake mkubwa wa kike, Faezah Rafsanjani ambaye amekuwa iakiunga mkono hadharani maandamano hayo sasa wameachiliwa huru.


Naye kiongozi wa upinazni Mir Hossein Mousavi ameapa kwamba ataendelea kusimama upande wa wale wote wamekuwa wakijitolea majiani kulilia haki yao iheshimiwe, lakini ameongeza kwamba hatokubali kuyahatarisha zaidi maisha ya waandamanaji hao na kuwashtumu maafisa wa usalama akiwaambia damu wanayoimwaga ni ya wenzao.


Katika Tovuti yake ya Internet Moussavi ametoa wito kwa wafuasi wake waendelea kutetea kile anachosema ni haki yao. Wafuasi wake pia wamewataka watu leo wajitokeze na kubeba mishumaa mieusi, kama kumbukumbu ya wale waliouawa katika machafuko haya.


Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE, AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman