1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa Al Jazeera wahukumiwa kifungo

29 Agosti 2015

Mahakama Misri (Jumamosi 29.08.2015) imewahukumu waandishi watatu wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera kifungo cha miaka 3 gerezani kwa kufanya kazi bila ya leseni na kutangaza habari ambazo zina madhara kwa Misri.

https://p.dw.com/p/1GNox
Waandishi wa Al Jazeera Baher Mohamed (kushoto) Mohammed Fahmy(katikati) na Peter Greste(kulia).
Waandishi wa Al Jazeera Baher Mohamed (kushoto) Mohammed Fahmy(katikati) na Peter Greste(kulia).Picha: picture-alliance/AP Photo

Hukumu hiyo imetolewa katika marudio ya kesi dhidi ya Mohamed Fahmy ambaye ameuacha uraia wake wa Misri na kuchukuwa wa Canada, Baher Mohamed raia wa Misri na Peter Greste raia wa Australia ayerudishwa kwao hapo mwezi wa Februari.

Jaji Hassan Farid amesema washtakiwa hao "sio waandishi wa habari na sio wanachama wa shirika la habari " na kwamba walikuwa wakitangaza bila ya kuwa na leseni.

Baher ameongezewa kifungo cha miezi sita gerezani. Shirika la habari la serikali MENA limesema imebidi aongezewe muda wa kifungo kwa sababu alikuwa na risasi wakati wa kukamatwa kwake.

Afadhaishwa na hukumu

Waandishi hapo awali walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka saba hadi kumi gerezani kwa mashtaka yenye kujumuisha uenezaji wa uongo,kulisaidia kundi la kigaidi ikimaanisha Kundi la Udugu wa Kiislamu ambalo jeshi ililipinduwa madarakani miaka miwili iliopita.

Mwandishi Peter Greste ambaye amerudishwa kwao Australia mwezi wa Februari.
Mwandishi Peter Greste ambaye amerudishwa kwao Australia mwezi wa Februari.Picha: picture-alliance/dpa/F. Arrizabalaga

Washtakiwa hao wamekanusha mashtaka yote hayo kwa kuyaita kuwa ya upuuzi na wanaharakati wa haki za binaadamu wanasema kukamatwa kwao ni sehemu ya ukandamizaji wa uhuru wa kutowa maoni tokea jeshi lilipompinduwa Rais Mohamed Mursi ambaye ni kiongozi mwandamizi wa kundi la Udugu wa Kiislamu hapo mwezi wa Julai mwaka 2013 kufuatia kukamatwa kwa umma wa watu kutokana na utawala wake.

Akizungumza na Al Jazeera kuhusiana na hukumu hiyo Greste amesema amefadhaishwa na ukali wa hukumu hiyo amesema " Maneno kwa kweli hayatendi haki " na kwamba "Kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu ni fedheha.Kwa kweli imenivuruga"

Juhudi za kuwatowa gerezani

Kwa mujibu wa Marwa Omara mke wa Fahmy, mume wake na Mohamed ambao walikuwa wameachiliwa kwa dhamana hapo mwezi wa Februari baada ya kuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja wamerudishwa tena kizuizini baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.Omara alikuwa akitokwa na machozi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Mwandishi Mohammed Fahmy akisalimiana na mwanasheria wa haki za binaadamu Amal Clooney mahakamani Cairo .(29.08.2015)
Mwandishi Mohammed Fahmy akisalimiana na mwanasheria wa haki za binaadamu Amal Clooney mahakamani Cairo .(29.08.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo

Amal Klooney wakili wa Fahmy amekaririwa akisema "tutaikatia rufaa hukumu hii na tunataraji itatenguliwa.Hivi sasa tunafanya mikutano kadhaa na maafisa wa serikali ambapo tutaomba kurudishwa Canada haraka kwa Bw.Fahmy."Amesema mwenzake Peter Greste alirudishwa Australia hakuna sababu jambo hilo hilo lisifanyike kwa kesi ya Fahmy.

Serikali za mataifa ya magharibi zimeelezea wasi wasi kuhusu uhuru wa kuzungumza nchini Misri tokea kupinduliwa kwa Mursi lakini hazikuchukuwa hatua madhubuti kuendeleza demokrasia nchini humo nchi ambayo ni mshiriika mhumimu.

Mke wa Fahmy adai haki

Mke wa Fahmy amesema hiyo sio haki kabisa na kwamba Mohamed ndio ameshahukumiwa kile anachoweza kuomba kwa sasa ni kwa wenzake wote kusimama naye na kuendelea kutowa wito wa kuachiliwa kwake.

Mwandishi Mohamed Fahmy katika mojawapo ya mchakato wa kesi yake.
Mwandishi Mohamed Fahmy katika mojawapo ya mchakato wa kesi yake.Picha: picture-alliance/AP Photo

Ameitaka serikali ya Canada kumrudisha nyumbani mume wake huyo kwa kuwa ni raia wa Canada na kwamba kitu pekee anachoomba ni haki na usawa, kilichotokea kwa Peter kitumike pia kwa Mohamed.

Al Jazeera imelaani uamuzi huo wa mahakama katika taarifa iliyosomwa na mkurugenzi mkuu wa kituo hicho Mustafa Sawaq."Hukumu hii ni shambulio jipya kwa uhuru wa vyombo vya habari na ni siku ya kiza katika historia ya haki nchini Misri."

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yameishutumu Misri kwa kuuurudisha nyuma uhuru waliopata kutokana na uasi wa umma wa mwaka 2011 ambao ulimuangusha Hosni Mubarak.

Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu Amnesty International na Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka yamelaani hukumu hiyo ya kuwafunga gerezani waandishi hao wa Al-Jazeera.

Mwandishi : Mohamed Dahmn /Reuters/dpa

Mhariri : Isaac Gamba