1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa Ethiopia wanadai Uhuru wao

MjahidA14 Mei 2013

Vyombo mbali mbali vya habari nchini Ethiopia vimekutana pamoja kuunda Baraza la habari vikiwa na matumaini ya kupunguza mipaka inayowekewa waandishi habari nchini Humo

https://p.dw.com/p/18X1L
wanahabari
wanahabariPicha: AP

Waandishi walipendekeza wazo hilo katika mkutano uliofanyika wiki iliyopita chini ya wizara ya habari na mawasiliano kuzungumzia mabadiliko ya vyombo vya habari katika taifa hilo la Afrika.

Kulingana na Getachew Worku, mhariri wa gazeti binafsi la Ethio Mihidar huu ulikuwa mkutano wa kwanza na wa kipekee ambapo waandishi habari na serikali wamekuwa wazi katika maswala ya habari. “Lazima tukubali maendeleo kama haya ikiwa ni njia moja muhimu au mwelekeo mzuri katika kupunguza vizingiti katika sekta ya uandishi,” Alisema Worku.

Changamoto bado ni nyingi kwa wanahabari

Mhariri huyo amesema bado kuna changamoto nyingi kwa vyombo vya habari kufanya kazi yao kwa uhuru, akitoa mfano kwamba hadi leo mwandishi habari hawezi kutumia viwanda vya serikali vya uchapishaji kuweza kuchapisha habari zake, kwamba ni lazima atumie kampuni binafsi katika kuchapisha gazeti lake.

Getachew Worku anasema hatua hiyo inawagharimu sana ikizingatiwa kuwa magazeti ya serikali yanachapishwa kwa gharama za chini na kuepuka kufilisika.

Worku amesema tatizo kuu ni kwamba, unaweza kuandika kuhusu fashoni na habari za sanaa lakini inakuwa vigumu sana kuandika juu ya siasa kwa sababu ni tabu kupata leseni ya kuandika mambo ya siasa na mwandishi anapata mbinyo mkubwa kutoka kwa maafisa husika.

Ramani ya Ethiopia
Ramani ya Ethiopia

Baraza hilo la habari litaundwa na wahariri wa magazeti ya serikali na binafsi. Jukumu la baraza hilo ni kufanya majadiliano juu ya mipaka iliowekwa kwa waandishi nchini humo na pia kuhakikisha kuwapo na majadiliano ya moja kwa moja na ya kila mara na serikali juu ya suala hilo.

Kwa upande wa serikali, Shimeles Kemal afisa kutoka wizara ya habari amesema wamekuwa na mazungumzo yalio na tija. Shimeless amesema waandishi habari walitoa hoja nzuri za kujikosoa wao wenyewe na pia kuikosoa serikali na watatilia maanani kila kilochozungumzwa na kutoa majibu ya haraka huku kukiendelea kuwa na uhusiano mzuri kati ya pande hizo mbili.

Baadhi ya waandishi kukosa matumaini

Hata hivyo kando na ahadi hizo kutoka kwa serikali baadhi ya waandishi hawana matumaini ya kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia. Akizungumza na shirika la habari la IPS, Anania Sorri amesema anaamini serikali imekubali kuwa na mazungumzo na waandishi na kuridhia pendekezo la kuunda baraza la habari kwaajili ya kujaribu kuzima juhudi za wanahabari kutaka mabadiliko ya kweli.

Rafiki yake Sorri, Reeyot Alemu, ambaye ni mshindi wa tuzo ya uhuru wa wanahabari mwaka huu anatumikia kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya kupanga njama za kigaidi, ubadhirifu wa fedha na kufanya kazi na mashirika ya kigaidi. Baada ya rafiki yake kukata rufaa, makosa mawili yalifutiliwa mbali na kifungo chake kupunguzwa hadi miaka mitano jela.

Sorry amesema rafiki yake ana matatizo ya afya yakiwemo uvimbe katika titi lake, pua na tumbo na hivi karibuni maafisa katika gereza anakotumikia kifungo chake wamemuonya dhidi ya kulezea hali halisi ya gereza hilo kwa wageni wanaomtembelea. Reeyot Alemu aliambiwa pindi habari hizo zitakapotoka nje atawekwa katika kifungo cha peke yake yani atatengwa na wafungwa wengine.

Mwandishi habari Johan Persson aliyefungwa kwa madai ya kuunga mkono Ugaidi
Mwandishi habari Johan Persson aliyefungwa kwa madai ya kuunga mkono UgaidiPicha: dapd

Kutokana na mambo haya Sorri anasema haoni serikali ikibadilika na kutimiza matakwa ya wanahabari nchini Ethiopia. Mashirika ya kimataifa pia yamekuwa mstari wa mbele katika kuikosoa serikali ya Ethiopia kwa jinsi inavyowatendea waandishi wa ndani ya nchi hiyo. Kulingana na kamati inayowalinda wanahabari, kwa sasa wanahabari saba wanaendelea kubakia gerezani huku waandishi wengi wakiitoroka nchi hiyo. Tangu mwaka wa 2001 waandishi 79 wameikimbia nchi hiyo kufuatia tatizo la uhuru wa wanahabari.

Lakini huku wanahabari wakijaribu kuunda baraza lao na kutumai kwamba litaleta mabadiliko katika kupatikana uhuru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia, hali halisi inabakia kwamba bado wanahabari katika nchi hiyo wanakibarua kigumu cha kuhakikisha uhuru wao unapatikana.

Mwandishi: Amina Abubakar/IPS

Mhariri: Sekione Kitojo