1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi wa nchi za umoja wa kiarabu kuzuru vitovu vya ghasia nchini Syria

29 Desemba 2011

Vikosi vya usalama vya Syria vimewauwa raia 14 zaidi huku waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu wakitarajiwa leo kuyazuru maeneo zaidi yanayoshuhudia machafuko.

https://p.dw.com/p/13bHg
Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji Syria
Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji SyriaPicha: dapd

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Uingereza, Syrian Observatory for Human Rights, takriban wanajeshi saba, wanne wakiwa watiifu kwa rais Bashar al Assad na watatu walioiasi serikali, waliuwawa jana katika mapambano tofauti.

Mtoto mwenye umri wa miaka mitano ni miongoni mwa raia wanne waliouwawa na vikosi vya usalama mjini Homs, huku waangalizi wa Kiarabu wakizuru maeneo jirani ya mji huo wa Homs kwa siku ya pili.

Hii leo waangalizi hao watazuru mikoa ya kaskazini ya Idlib na Hama pamoja na Daraa kusini mwa nchi hiyo, ambako ndio kitovu cha maandamano ya kutaka demokrasia yalikoanzia mwezi Machi.

Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa jumuiya ya Kirabau Jenerali Mohammed Ahmed Mustafa al Dabi amesema pia watazuru mji mkuu Damascus. Kulingana na watetezi wa haki za binadamu raia watatu waliuwawa na wanajeshi wa Syria waliowafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiupinga utawala wa rais Assad katika mji wa kaskazini wa Hama. Raia mwingine pia aliuwawa katika mji wa Aleppo, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa kiuchumi nchini Syria, huku mwingine akiuwawa katika mkoa wa Idlib unaopakana na Uturuki, naye wa tatu akauwawa katika mji wa Daraa alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye maandamano.

Ujumbe wa nchi za kiarabu utachukua muda wa mwezi mmoja nchini humo, ambao kulingana na mkataba uliotiwa saini na Syria, unaweza kurefushwa. Kufikia sasa kuna waangalizi 66 lakiini mkuu wa ujumbe huo anasema idadi yao itaongezeka wakati wakizidi kuyazuru maeneo mengine mengi kote nchini humo.

Waandamanaji nchini Syria wakiwa na mabango ya kuupinga utawala wa rais Bashar al Assad
Waandamanaji nchini Syria wakiwa na mabango ya kuupinga utawala wa rais Bashar al AssadPicha: dapd

Wakati huo huo China imetangaza kuwaunga mkono waangalizi wa umoja wan chi za Kiarabu nchini Syria baada ya Ufaransa kudai kuwa ujumbe huo haujakubaliwa kuona kile kinachoendelea katika mji unaokabiliwa na ghasia wa Homs.

China ni mshirika mkuu wa Syria na pamoja na Urusi imetumia kura yake ya turufu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kuzuia azimio linaloungwa mkono na mataifa ya magharibi linalomlaani rais wa Syria Bashar al Assad. China inataraji kuwa pande husika zinaweza kushirikiana katika juhudi za kuutekeleza mkataba wa ujumbe huo ili kutafuta suluhu la kuumaliza mzozo huo wa Syria.

Nazo Ufaransa na Marekani imesema kuwa waangalizi hao ni sharti wapewe fursa ya kuingia ndani hadi katika maeneo yanayoshuhudia umwagikaji wa damu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu