1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alassane Ouattara anaelekea kupata ushindi

27 Oktoba 2015

Uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Cote d'Ivoire mwishoni mwa wiki umepata sifa kutoka kwa waangalizi kuwa ulikuwa wa amani na huru. Lakini upinzani umepinga idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki

https://p.dw.com/p/1GuiX
Präsidentschaftswahl in der Elfenbeinküste - Alassane Ouattara
Picha: DW/K. Gänsler

Uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Cote d'Ivoire mwishoni mwa wiki umepata sifa kutoka kwa waangalizi kuwa ulikuwa wa amani na huru. Lakini upinzani umepinga idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi huo wakati taifa hilo la Afrika magharibi likijaribu kujikwamua kuondokana na historia ya machafuko ya uchaguzi.

Rais wa sasa wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara alifahamu kabla kuwa idadi kubwa ya wapiga kura ingetosha kumpa ushindi katika uchaguzi huo anaopigiwa upatu kushinda. Lakini wakati makadirio ya mwanzo kutoka tume ya uchaguzi yakisema idadi ya wapiga kura ilikuwa “karibu asilimia 60”, makundi ya kiraria yamesema ilikuwa chini kidogo, asilimia 53.

Präsidentschaftswahl in der Elfenbeinküste Stimmauszählung
Matokeo ya uchaguzo wa Cote d'Ivoire yanasubiriwaPicha: Reuters/T. Gouegnon

Hata hivyo, muungano wa upinzani wa CNC, unaowawakilisha wagombea wawili wa urais, wameweka idadi huyo kuwa chini ya asilimia 20, na kuuita uchaguzi huo kuwa ni “kejeli” na makadirio rasmi “yasiyowezekana”.

Waangalizi walitarajia ushiriki kuwa mdogo kulikuwa wakati Ouattara aliposhinda uchaguzi wa mwisho mwaka wa 2010, huku baadhi ya wapinzani wakitoa wito wa kususia na wagombea watatu wakuu kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho. Msemaji wa Ouattara Joel N'Guessan ameyapuuzilia mbali madai ya upinzani, akisema tabia yao “siyo ya heshima na kuwajibika” na wasiotaka kukubali kushindwa.

Katika mwaka wa 2010, idadi ya wapiga kura ilikuwa kubwa mno, kwa sababu uchaguzi uliahirishwa mara sita na nchi ilikuwa imegawika mara mbili.

Ulifuatwa na miezi kadhaa ya machafuko ambayo karibu watu 3,000 waliuawa. Kinyume chake siku ya Jumapili, ijapokuwa vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kuchelewa kutokana na kuchelewa kuwasili kwa vifaa na kompyuta za tablet zilizotumiwa kuangalia vitambulisho vya wapiga kura zikashindwa kufanya kazi, hakuna matatizo makuu yaliyoripotiwa na waangalizi kwa ujumla wameuona uchaguzi huo kuwa wa haki.

Nigeria Bildergalerie Staatspräsidenten Olusegun Obasanjo
Rais wa Zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ni kiongozi wa waangalizi wa ECOWASPicha: Chung Sung-Jun/Getty Images

Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, aliyeongoza timu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi – ECOWAS amesema uchaguzi huo utaonyesha mapenzi ya watu wa Cote d'Ivoire.

Kouadio Konan Bertin, mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, amekiri kushindwa hapo jana na kumpongeza Ouattara kwa ushindi anaodhaniwa kuupata.

Waangalizi wa Umoja wa Afrika wamekubali kuwa uchaguzi huo uliendeshwa vyema. Waziri Mkuu wa zamani wa Senegal Aminata Traore aliyeonngoza ujumbe wa uangalizi wa Umoja wa Afrika amesema kwa mujibu wa walichokiona, shughuli hiyo ilifanywa kwa njia ya uwazi.

Ubalozi wa Marekani mjini Abidjan umetoa taarifa ukiwapongeza raia wa Cote d'Ivoire kwa kuandaa uchaguzi ulioonekana kuwa wa “amani, uwazi, halali na uliowajumuisha watu wote”. Taarifa hiyo imesema inatumai matokeo ya duru ya kwanza, yatakapotanzwa, yatakubalika na wote waliogombea kwenye uchaguzi huo. Matokeo ya upigaji kura huo yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri:Josephat Charo