1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Libya wameushambulia mji wa Ghazaya

28 Julai 2011

Kiongozi wa Libya anaendelea kukaidi kuondoka madarakani wakati waasi hii leo wameanzisha mashambulio kwa mji unaodhibitiwa na serikali uliopo karibu na mpaka wa Tunisia

https://p.dw.com/p/125SW
Shambulio la roketi la waasi nchini LibyaPicha: dapd

Kanali Muammer Gaddafi amesema yuko tayari kujitolea maisha yake kuwashinda waasi wanaopigana na vikosi vyake baada ya wao kutoa onyo kuwa muda wa mwisho wa kiongozi huyo kujiuzulu na kuishi nchini Libya umemalizika.

Rebellen in Libyen
Mojawapo ya waasi nchini humoPicha: DW

Katika ujumbe aliotoa hapo jana jioni kwa wafuasi wake kwenye mji wa Zlatan uliopo karibu na mpaka wa Tunisia, Kanali Muammer Gaddafi amesema kuwa wako tayari kujitolea maisha yao ya wake na watoto wao katika kujitolea kumshinda adui.

Gaddafi pia alitoa wito kwa wafuasi wake kuandamana hadi katika eneo la Nafusa linalodhibitiwa na waasi katika eneo lililo na milima, kusini magharibi mwa mji mkuu Tripoli, na kutoa wito kwa wapinzani wake wasalimu amri. Aliongeza kuwa bila ya usaidizi wa shirika la kujihami NATO, waasi hao hawangefanikiwa kulidhibiti eneo hilo la milimani.

Waasi wanalitumia eneo la Nafusa kama mwanzo wa uvamizi wao wa mji mkuu ili kuupindua utawala wa Gaddafi.

Libyen / Gaddafi / Tripolis
Kanali Muammer GaddafiPicha: AP

Hii leo (28.07.11) msemaji wa waasi nchini Libya, Mohammed Maylud ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wameanza kuushambulia mji wa Ghazaya kwa maroketi na vifaru na kuongeza kuwa waasi hao walivishambulia vijiji vingine vinne vilivopo kwenye milima iliopo magharibi mwa Libya.

Vikosi vya Gaddafi vinaudhibiti mji huo na vinautumia kama kambi ya kuushambulia mji unaodhibitiwa na waasi, Nalut, na pia waasi waliopo katika eneo karibu na mpaka wa Tunisia.

Eneo la milima la Nafusa limeshuhudia mapigano makali kati ya waasi na wafuasi wa Gaddafi.

Wakati huo huo kufuatia hatua ya Uingreza hapo jana kuwafukuza wanadiplomasia katika ubalozi wa Libya nchini humo na kuwatambua waasi kuwa ndio uongozi halali wa Libya, mwenyekiti wa baraza la mpito la waasi,Mustafa Mohammed Abdel Jalil, aliikaribisha hatua hiyo na baraza hilo linatarajia Uingereza na Uturuki kuwa nchi za kwanza kuachia sehemu ya mali za Libya zilizo zizuia.

Mustafa Abdul Jalil Ex-Justizminister Libyen
Mwenyekiti wa baraza la mpito la waasi nchini Libya, Mustafa Abdul JalilPicha: picture alliance/dpa

Abdel Jalil, amesema kuwa waasi hao waliwasilisha pendekezo lenye nia nzuri kwa mjumbe maalum wa umoja wa mataifa, Abdullah Al Khatib, kuwa Gaddafi anaweza kuishi nchini Libya kwa masharti matatu.

Chini ya masharti hayo, Gaddafi angetakiwa kujiuzulu, na kuachia madaraka yote, wananchi wa Libya wataamua makaazi yake yaweko wapi, na atakua akichunguzwa kwa karibu mno. Muda uliowekwa sasa umepita, na Gaddafi amekula kiapo kutosalimu amri.

Mwandishi Maryam Abdalla/Afpe/Rtre/
Mhariri: Abdul-Rahman