1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Syria wadungua helikopta

Admin.WagnerD27 Agosti 2012

Waasi wa Syria wamesema wameiangusha helikopta ya jeshi la serikali wakati ikifanya mashambulizi katika viunga vya mji mkuu, Damascus, huku mapigano makali yakiendelea kuripotiwa katika sehemu kadhaa za nchi.

https://p.dw.com/p/15xGK
Helikopta ya jeshi la serikali ya Syria
Helikopta ya jeshi la serikali ya SyriaPicha: Reuters

Helikopta hiyo imeanguka karibu na msikiti wa Qaboon katika kitongoji vya Jubar kilichoko mashariki mwa mjini mkuu wa Syria, Damascus, na ambacho wakazi wake wengi ni wapinzani wa serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Ilikuwa ikitumiwa kuwashambulia wapiganaji wa kile kinachojulikana kama Jeshi Huru la Syria, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lililo na makao nchini Uingereza. Jeshi Huru la Syria ambalo tarehe 13 mwezi huu lilitangaza kuiangusha ndege ya kivita ya serikali, limedai kuiangusha pia helikopta hiyo.

Shutuma za mauaji ya maangamizi

Mashambulizi makali dhidi ya waasi yameanzishwa siku moja baada ya wanaharakati wa upinzani kuishutumu serikali ya Rais Assad kufanya mauaji mengine ya maangamizi katika mji wa Daraya ulioko kusini magharibi mwa nchi.

Mamia ya watu wameuwa katika mji wa Daraya
Mamia ya watu wameuwa katika mji wa DarayaPicha: dapd

Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lilisema kuwa zaidi ya maiti 300 ziligunduliwa katika mji mdogo wa Wasunni baada ya mji huo kushambuliwa vikali kwa mizinga kwa muda wa siku tano, na msako wa nyumba kwa nyumba ambao ulifanywa na wanajeshi wa serikali.

Shirika hilo limesema leo kuwa maiti 14 zaidi zimegunduliwa katika mji huo huo wa Daraya, baada ya tangazo la jana kuwa waliouawa walikuwa watu 320.

Kamati za wanaharakati walioko ndani ya Syria zimesema kwamba maiti za watu waliouawa zilichomwa moto na wanamgambo wa Shabiha ambao ni washirika wa serikali, na ambao kamati hizo zinasema wamegeuzwa kuwa "mashine za mauaji."

Uingereza imesema kuwa endapo mauaji hayo yatathibitishwa, yatakuwa ni msiba wa kiwango kipya. Vyombo vya habari vya serikali vimewalaumu waasi ambao vinawaita magaidi, kufanya mauaji hayo ya raia.

Msimamo wa serikali ni ule ule

Licha ya shutuma hizi lakini, Rais Assad ameapa kutobadilisha msimamo wake dhidi ya kile alichosema ni hila za nchi za magharibi na baadhi ya majirani wa Syria. Alisema, ''Watu wa Syria, kamwe hawataruhusu njama hizo kufikia malengo yake, na watazishinda kwa gharama yoyote ile.''

Rais Bashar ameapa kuwapiga vita waasi hadi ushindi upatikane
Rais Bashar ameapa kuwapiga vita waasi hadi ushindi upatikanePicha: picture alliance/dpa

Rais Assad aliyasema hayo akizungumza na makamanda wa kijeshi kutoka Iran, ambayo ni mshirika wake mkuu katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Kuanzia mwezi Machi mwaka jana, Assad amekuwa akitumia nguvu za kijeshi kujaribu kuukandamiza upinzani, na ghasia zilizofuatia zimeitumbukiza Syria katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimeuwa maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine laki mbili kuikimbia nchi yao. Wengine wapatao milioni 2.5 ndani ya Syria wanahitaji msaada.

Waasi wang'ang'ana

Jeshi la serikali lina nguvu na zana bora zaidi za kivita, lakini linapata matatizo kuwang'oa wapinzani, ambao wamejizatiti katika ngome zilizoko katika maeneo mengi ya nchi, hususan katika mji wa kaskazini wa Aleppo.

Wakati hayo yakiarifiwa, mkuu wa kamati ya sera za nje katika bunge la Iran, Aladin Borujerdi, amesema kuwa Iran haitamtupa mkono Assad, ambaye alimtaja kama ndugu. Kauli yake aliitoa wakati akikutana na Rais Assad pamoja na makamu wa Rais Faruk al-Sharaa mjini Damascus. Makamu huyo wa raisi alikuwa hapo mwanzoni ameripotiwa kuukimbia utawala wa Assad na kujiunga na wapinzani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef