1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Houthi wayateka maeneo zaidi Yemen

Admin.WagnerD14 Oktoba 2014

Waasi nchini Yemen wameuteka mji muhimu wa bandari na kutanua maeneo wanayoyadhibiti nchini humo.Hayo yanakuja siku moja tu baada ya waziri mkuu mpya kutangazwa katika juhudi za kuutatua mzozo wa kisiasa nchini humo

https://p.dw.com/p/1DVYf
Picha: REUTERS/K. Abdullah

Afisa mmoja wa serikali ya Yemen amesema waasi wa kishia wa Houthi hawakupata upinzani mkubwa walipouteka mji wa Hudeida, huu ukiwa mji wa pili wa bandari nchini Yemen kuangukia mikononi mwa waasi na kuongeza waasi hao wako katika vituo muhimu vya nchi hiyo vikiwemo viwanja vya ndege na bandari.

Duru kutoka jeshi la Yemen pamoja na kutoka kwa waasi hao zimethibitisha kuwa wanamgambo wa Houthi wameonekana wakishika doria katika barabara kuu katika mji huo ambao una zaidi ya wakaaazi milioni mbili.

Waasi wanavidhibiti pia vituo muhimu

Walioshuhudia wamesema waasi hao waliweka vizuizi katika vituo vyote vikuu vya kuingia mjini humo huku ikiripotiwa askari mmoja ameuawa wakati waasi hao walipoyateka majengo ya mahakama.

Mji wa Hudaida,Yemen
Mji wa Hudaida,YemenPicha: picture-alliance/dpa/Angela Merker

Afisa wa eneo hilo amesema wanamgambo wa Houthi walishambulia bohari moja la kutunzia silaha karibu na mji wa Hudeida kabla ya kuushambulia mji huo.

Hayo yanakuja wiki chache tu baada ya waasi hao kuuvamia mji mkuu Sanaa ulioko kilomita 220 mashariki mwa mji huo.Taifa hilo limekumbwa na msukosuko wa kisiasa na ghasia za mara kwa mara tangu kung'olewa madarakani kwa kiongozi wa kiimla Ali Abdullah Saleh mwaka 2012.

Wanamgambo wa makundi mabli mbali wamekuwa waking'angania kutumia fursa ya kuwepo pengo la uongozi nchini humo kufikia maslahi yao.Wengi wa waasi hao wamekuwa wakiendeleza uasi kaskazini mwa nchi hiyo lakini katika miezi ya hivi karibuni wametanua uasi huo katika juhudi za kulidhibiti taifa hilo.

Duru za kijeshi zilionya awali kuwa waasi hao wanapania kuuteka mji wa Hudeida na kutanua udhibiti wao hadi mlango wa bahari wa Bab al Mandab eneo linaloekea mfereji wa Suez.

Kulingana na idara ya taarifa kuhusu nishati ya Marekani,mlango huo wa bahari ulitumika kusafirisha mapipa ya mafuta milioni 3.4 mwaka 2011

Udhaifu serikalini wawapa waasi nguvu

Waasi wa Houthi wanasemekana hivi sasa kuutupia macho mji wenye utajiri wa gesi na mafuta wa Marib na kuzua hofu kuwa waasi hao wamekusudia kuunda taifa lao dogo ndani ya Yemen ikizingatiwa kuwepo udhaifu serikalini na katika usimamizi wa vikosi vya usalama.

Waziri Mkuu mpya wa Yemen Khaled Bahah
Waziri Mkuu mpya wa Yemen Khaled BahahPicha: Reuters/Khaled Abdullah

Wachambuzi wa Yemen wanasema kundi la Houthi ambalo linashukiwa kuungwa mkono na Iran huenda limechochewa zaidi na ufanisi wao wa kuuteka mji mkuu wa Sanaa na hivyo kupata nguvu za kuendelea kuiteka miji zaidi.

Mbali na Sanaa,pia wanayadhibiti majimbo ya Saada na Moran kaskinzini mwa nchi huyo na kusini mw Yemen wamelidhibiti jimbo la Damar ambako askari na wanajeshi waliutoroka baada ya waasi hao kuwasili.

Huku hayo yakijiri,maelfu ya watu wameandamana leo katika mji wa Aden kutaka kujitenga kutoka eneo la kaskazini mwa Yemen.Yemen Kusini lilikuwa taifa huru hadi lilipounganishwa na Yemen kaskazini mwaka 1990.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman