1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wadai kusonga Mbele Libya.

17 Agosti 2011

Waasi nchini Libya wanadai kusonga mbele kuelekea ngome ya kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, Tripoli, baada ya kufanikiwa kuudhibiti mji alikozaliwa kiongozi huyo uliyopo kati ya miji ya Tripoli na Sirte.

https://p.dw.com/p/12IBB
Waasi wakiwa wamefunga barabara ya kuelekea TripoliPicha: DW

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, kamanda wa majeshi ya waasi ameoneshwa akitangaza kuwa, vikosi vya ukombozi vimefanikiwa kuwafurusha wanajeshi wa Gaddafi kutoka katika mji wa al-Heesha, uliyopo kilometa 140 magharibi mwa Sirte.

Mapema wiki hii, waasi walisema walifanikiwa kusonga mbele mpaka katikati ya mji wa bandari muhimu ya mafuta wa Zawiya, mji huo upo umbali wa kilometa 40 magharibi mwa Tripoli.

Leo hii Al-Jazeera imearifu kwamba, waasi wamefanikiwa kumkamata kiongozi wa usalama wa Zawiya na viongozi wengine katika utawala wa Gaddafi akiwemo afisa mwandamizi wa jeshi.

Dossierbild 1 Libyen Rebellen
Waasi wakishangilia baada ya kuingia BregaPicha: dapd

Wanajeshi wa Gaddafi ambao kwa hivi sasa wanadhibiti upande wa magharibi kuelekea Tripoli wameonekana wakipambana kuurejesha mji huo katika himaya yao.

Watunguaji wameonekana wakiwa katika mapaa ya nyumba wakifanya shughulia yao ya utunguaji huku, mji ukitingishwa na milio ya maroketi na mizinga.

Shirika la Habari Uingereza Reutes limearifu kwamba kiasi ya watu watatu wameuwawa na wengine 35 kujeruhiwa katika mapigano yaliyotokea jana.

Kwa upande wao waasi wamefunga njia kubwa muhimu ya kupeleka mahitaji muhimu na bidhaa nyingine nchini Libya, kutokea nchi jirani ya Tunisa.

Wakati huo huo Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Abdul Illah al-Khatib, amekanusha taarifa za kuendesha mazungumzo ya pamoja ya upatanishi kati ya pande hasimu nchini humo.

Al-Khatib amesema amefanya mikutano tofauti kwa pande zote mbili na baadhi ya wananchi wa Libya kutokana na maombi yao.

Hapo jana Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Waasi, Mustafa Abdul Jalil alithibitisha kwamba hakuna mazungumzo yeyote ya upatanishi yaliyofanyika kati yao na serikali ya Gaddafi.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Benghazi, Jalil aliongeza kuwa " Gaddafi anapaswa kujiuzulu na kuondoka Libya au ataondolewa kwa nguvu"

Waasi wamekuwa wakipambana kwa wiki kadhaa sasa kuelekea Tripoli. Wamekuwa wakihangaika kumuondoa Gaddafi madarakani tangu Februari, na hivi karibuni wakidai kupiga hatua kubwa katika mji wenye hazina ya mafuta wa Brega uliyopo kilometa 750, mashariki mwa Tripoli.

Mwandishi: Sudi Mnette/ RTR/DPA
Mhariri:Josephat Charo