1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wajiandaa kushambulia Bani Walid

5 Septemba 2011

Mazungumzo ya kushinikiza kusalimu amri kwa majeshi ya Gaddafi kwenye ngome ya mwisho ya kiongozi huyo katika mji wa Bani Walid yameshindikana na hayawezi kufanyika tena, jambo ambalo linaweza kuanzisha mapigano.

https://p.dw.com/p/12TBk
Wapiganaji waasi wakifanya doriaPicha: dapd

Mazungumzo ya kushinikiza kusalimu amri kwa majeshi ya Gaddafi kwenye ngome ya mwisho ya kiongozi huyo katika mji wa Bani Walid yameshindikana na hayawezi kufanyika tena, jambo ambalo limefungua milango ya kufanyika kwa mashambulizi ya kijeshi muda wowote kuanzisha sasa.

Mpatanishi wa Seriakali mpya ya Baraza la Mpito la Waasi-NTC, Abdullah Kenshil, alinukuliwa na Shirika la Habari la Ufaransa-AFP- akisema " namwachia kamanda wa kijeshi kutatua tatizo"

Bani Walid, mji uliopo kusini mashariki ni moja kati ya ngome za mwisho za wapiganaji wa Gaddafi ambayo inahisiwa kwamba mmoja kati ya watoto wa Gaddafi amejificha.

Libyen Deutschland Gewehre Waffen Heckler und Koch G36
Mpiganaji muasiPicha: picture-alliance/dpa

Kenshil alisema upande wa Gaddafi ulitaka wapiganaji waasi waingia katika mji huo bila ya silaha jambo ambalo halikuridhiwa kutokana na kuonekana kama ghiliba.

"Dakika ya mwisho kujaribu kutafuta muafaka katika mazungumzo haya tulirdhia mengi, hata kama mwanzo tulikataa kuzungumza na watu wenye mfungamano na utawala" alisema Keshil

Akizungumza pasipo kutoa maelezo ya kina, mpatanishi huyo alidai hata Gaddafi mwenyewe, watoto wake na baadhi ya wanafamilia wengine wapo katika mji huo wa Bani Walid.

Mazungumzo hayo, kwa kutumia viongozi wa kikabilia, yalianza siku chache zilizopita kwa lengo la kufanikisha upande wa waasi kudhibiti mji huo pasipo kumwaga damu.

Saadi Gaddafi amesema kushindikana kwa mazungumzo hayo kumesababishwa na kaka yake, Seif al-Islam, ambae anatafutwa na mahakama ya uhalifu wa kivita, sambamba na baba yake kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita.

Saadi aliyasema hayo wakati alipofanya mahojiano kwa njia ya simu na televisheni ya CNN ambapo alipoulizwa mahali alipo alijibu kwamba yupo maeneo ya karibu na Bani Walid.

Mtoto huyo wa Gaddafi, ambae alisema hafungamani na upande wowote, na yuko tayari kushiriki katiika jitihada za upatanishi, alidai hajaonana na kaka yake, Seif, wala baba yake kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Wakati huohuo, msemaji wa Jeshi la waasi, Ahmed Omar Bani, amethibitisha kifo cha mtoto mwingine wa Gaddafi, Khamis, pamoja na mtoto wa aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa wa nchi hiyo, Abdullah Senussi.

Akizungumza na waandhi wa habari mjini Benghazi, amesema wote kwa pamoja wameuwawa katika eneo la Tarhuna, mji uliopo kaskazini mwa Bani Walid.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri:Miraji Othman