1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wapigwa Chad

Kalyango Siraj18 Juni 2008

Wengine wachukuliwa mateka

https://p.dw.com/p/EMJl
Rais Idriss Deby wa Chad.Majeshi yake yawapa kipigo waasi.Picha: AP

Chad inasema imeweza kuzia waasi kutosonga mbele kuelekea mji mkuu wa Ndjamena katika juhudi zao mpya za kutaka kuung'oa utawala wa rais Idriss Deby,ambae kwa upande wake, anailaumu Sudan kwa kuwaunga mkono waasi hao.

Mkuu wa majeshi ya Chad,Generali Touka Ramadhan Kore ,leo jumatano amewambia maripota kuwa vijana wake wamewapa kipigo waasi katika eneo la Am Zoer,lilioko kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa mkoa wa mashariki wa Abeche.

Mkuu huyo ameongeza kuwa katika kipigo hicho jeshi la serikali limeweza kuwauwa waasi zaidi ya 160 na pia kuwazuia waasi hao kutosonga mbele kwa mara ya kwanza ,tangu waasi hao walipoanzisha hujuma zao mwishoni mwa juma.

Akiwaita waasi hao kama mamluki,mkuu wa majeshi ya Chad, amesema kuwa mamluki wa Sudan aidha wameuawa ama kukimbia na kuongeza kuwa wengi wamechukuliwa mateka.

Katika mapigano hayo, amesema, jeshi lake limepoteza wanajeshi watatu lakini kwa upande mwingine limefaulu kuyakomboa magari ya kijeshi 40 hivi yaliyokuwa yametekwa na waasi hao hapo kabla.

Kuthibitisha madai yake ya ushindi,Generali Kore amewaonyesha waandishi habari wafungwa wa kivita 20,ambapo watano kati yao walikuwa na majeraha waliyoyapata wakati wa mapambano.

Waasi hao walianzisha tena hujuma dhidi ya rais Idriss Deby Juni 11 kwa kushambulia miji midogomidogo minne ya mashariki mwa nchi hiyo kabla ya kusonga mbele.

Chad na Sudan zinalaumiana kwa kuwasaidia waasi wanaoipinga serikali ya nchi nyingine.

Wakati huu ambapo serikali ya Deby ikiulaumu utawala wa Khartoum kwa, sio tu kuwaunga mkono waasi kwa hali na mali, lakini pia,Gavana wa mkoa wa mashariki wa Chad wa Ouaddai, unaokaribiana na jimbo la Darfur,Generali Issa Djadallah Bichara anasema kuwa vikosi vya Sudan vimefanya mashambulio mara mbili ndani mwa Chad.

Uhusiano wa nchi hizo mbili ulivunjika mwezi Mei baada ya shambulio la waasi wa Darfur wa kundi la Justice and Equality Movement JEM dhidi ya mji wa Omdurman.Utawala wa Khartoum unadai waliungwa mkono na serikali ya Chad madai Ndjamena inayokanusha.

Kiongozi wa Chad,Idriss Deby mbali na kuilaumu Sudan kwa kuwasaidia waasi hao pia amelishutumu jeshi la Ulaya linalolinda wakimbizi wa Darfur katika eneo hilo la EUFOR kwa kushirikiana na waasi.

Mkuu wa sera wa Umoja wa Ulaya,Javier Solana, amekanusha madai hayo akisema jeshi hilo haliwezi kuegemea upande mmoja akiongeza kuwa shabaha ya jeshi hilo baado haijabadilika.

Chad, nchi ambayo ni ya tano kwa ukubwa barani Afrika,licha ya kuwa na utajiri wa mali asili kama vile dhahabu,Uranium pamoja na mafuta,lakini umaskaini ni mwingi nchini humo.Pia imezongwa na migogoro ya ndani kwa kipindi kirefu tangu mkoloni Ufaransa aondoke mwaka wa 1960.

Rais Deby alieingia madarakani mwaka wa 1990 kupitia mapinduzi ya kijeshi akisaidiwa na Ufaransa na Libya anakosolewa kwa ukiukaji wa haki za binadamu,kutoiheshimu katiba ya nchi,na pia kuwa utawala wake umejaa rushwa.