1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wapinga mkataba wa amani

Ramadhani Yusuf, Saumu15 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DOl0

ND'JAMENA




Waasi wa Chad wamepinga makubaliano ya amani kati ya Chad na Sudan wakisema wataendelea na kampeini zao za kumuondoa madarakani rais Idris Deby wa Chad.

Alhamisi Chad na Sudan zilitia saini huko mjini Dakar Senegal makubaliano ya kukomesha uhasama baina yao.

Kwa mujibu wa kamanda  mkuu wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur,mpango huo wa amani hauwezi kufanikiwa ikiwa waasi wa nchi zote mbili hawatahusishwa.

Msemaji wa kundi la waasi wa Chad amesema makubalaino ya amani yaliyotiwa saini kati ya rais Idriss Deby wa Chad na Omar El Bashir  wa Sudan hayawahusu bali wanataka mazungumzo ya moja kwa moja na rais wa Chad vinginevyo wataimarisha juhudi za kumtimua madarakani.Waasi wa Chad mwezi uliopita walipambana vikali na wanajeshi wa serikali kwa muda wa siku mbili kwenye mji mkuu Ndjamena katika jaribio la kumpindua madarakani rais Deby.Katika mapatano yaliyosainiwa alhamisi pembezoni mwa mkutano wa mataifa ya muungano wa nchi za kiislamu huko Senegal marais wa Chad na Sudan walikubaliana kuyakomesha makundi yenye silaha kutumia maeneo yaliyoko kwenye ardhi za nchi hizo mbili kutekeleza mashambulio.

Wakati huohuo Umoja wa mataifa umefahamisha kwamba unawarudisha wakimbizi zaidi katika eneo la kusini mwa Sudan.

Takriban watu laki mbili wameuwawa na zaidi ya wengine millioni mbili wameachwa bila makaazi katika kipindi cha miaka mitano ya mgogoro wa jimbo la Darfur.