1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wapuza makubaliano mapya ya amani

15 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DOxr

DAKAR:

Waasi wa Chad wameyapuuza makubaliano mapya ya amani yaliyotiwa saini na marais wa Chad na Sudan kwa kusema kuwa hayana umuhimu wala maana yo yote. Wakaongezea kuwa wataendelea kujaribu kumpindua Rais Idriss Deby wa Chad asietaka kujadiliano nao.Siku ya Jumatano, makundi ya waasi kwa mara nyingine tena yaliingia Chad kutoka Sudan.

Rais Deby na rais mwenzake wa Sudan,Omar Hassan al-Bashir siku ya Alkhamisi mjini Dakar walitia saini makubaliano ya kutoshambuliana.Lengo ni kukomesha mashambulizi ya waasi ndani ya nchi zao katika maeneo ya mpakani.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameyasifu makubaliano hayo kama ni hatua ya kuleta utulivu katika kanda hiyo na kuzuia mapambano katika jimbo la Darfur,magharibi mwa Sudan.Umoja wa Ulaya umeanza kupeleka vikosi vya amani-EUFOR kulinda usalama mashariki mwa Chad.Kiasi ya watu 500,000 waliopoteza makaazi yao wanaishi katika eneo hilo.Miongoni mwao pia kuna wakimbizi wa Darfur.