1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wasonga mbele kuelekea Tripoli

Aboubakary Jumaa Liongo6 Julai 2011

Waasi nchini Libya wakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya vikosi vya NATO inaarifiwa kuwa wako kiasi cha kilomita 50 kutoka mji mkuu Tripoli.

https://p.dw.com/p/11ppC
Waasi wa Libya katika uwanja wa mapambanoPicha: picture alliance / dpa

Taarifa hizo zinakuja huku mwanawe mkubwa kiongozi wa Libya Kanali Muhammar Gaddafi, akinukuliwa kusema kuwa baba yake yuko tayari kuingia katika majadiliano na waasi hao ili kuepusha umwagikaji zaidi wa damu.

Akinukuliwa na Shirika la habari la Ufaransa AFP kiongozi wa waasi hao amesema wanajeshi wake wakisaidiwa na operesheni za NATO wamekuwa wakisonga mbele ambapo wamefanya mashambulizi makali katika maeneo ya Gualish kwenye milima ya Nafusa kusini magharibi mwa mji mkuu Tripoli.

Mwandishi wa AFP aliyeko katika uwanja wa mapambano anasema kuwa kulikuwa na mapambano makali kati ya vikosi vya waasi na vile vitiifu kwa Kanali Gadafi.

Hapo kabla msemaji wa waasi hao Kanali Ahmed Omar Bani aliahidi kuwa mnamo siku chache zijazo hali katika uwanja wa mapambano itabadilika na kwamba watakuwa wakisonga mbele kuelekea Tripoli.

Naye Kamanda wa waasi hao Mokhtar Milad Fernana akizungumza na Deutsche Welle alisema kuwa wana uhakika kuwa mnamo kipindi cha wiki tatu zijazo watauteka mji huo mkuu.

Hapo siku ya Jumatatu Ufaransa ilikiri kuwapelekea silaha waasi hao, huku vikosi vya anga vya NATO vikizidisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo yenye silaha za jeshi la Libya, na hivyo kutoa urahisi kwa waasi hao kusonga mbele.

Lakini hapo jana Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Gerard Longuet alisema kuwa nchi hiyo haina haja tena ya kuwapatia silaha waasi hao kwani sasa wamejipanga vizuri.

Serikali ya Libya mara kadhaa imekuwa ikishutumu kuwa mashambulizi hayo yamekuwa yakilenga makaazi ya raia.Hata hivyo kiongozi wa Libya Kanali Muhammar Gaddafi ameyaonya mataifa ya Ulaya kuwa watalipiza kisasi kwa mashambulizi hayo.

NO FLASH Gaddafi Gadhafi Libyen Haftbefehl
Kiongozi wa Libya Muhammar GaddafiPicha: AP

´´Wananchi wa Libya wana uwezo wa kuutumbukiza mzozo huu katika bahari ya Mediterrania na kuupeleka Ulaya.Tuna uwezo wa kuingia katika majumba yenu, makazi yenu na familia zenu, maeneo ambayo kijeshi yatakuwa halali kushambuliwa, kama vile ambavyo mmegeuza ofisi zetu, nyumba zetu na watoto wetu kuwa maeneo halali kushambuliwa´´

Kwa upande mwengine mtoto mkubwa Kanali Gaddafi, Mohammed Gaddafi amemwambia mkuu wa shirika la mchezo wa Chess la Urusi Kirsan IIyumzhinov, kuwa baba yake yuko tayari kujadiliana na waasi hao ili kuumaliza mzozo huo uliyoigubika Libya tokea February mwaka huu.

Kirsan akizungumza mjini Moscow mara baada ya kurejea kutoka Libya ambako alikuwa huko kwa ziara ya siku tatu amesema mtoto huyo wa Gaddafi alimwambia kuwa baba yake yuko tayari kuingia katika majadiliano na waasi bila ya masharti yoyote.

Gazeti la New York Times la Marekani limesema kuwa mkuu huyo wa mchezo wa Chess nchini Urusi mjumbe asiye rasmi katika juhudi za Urusi kuushughulikia mzozo huo wa Libya.Hata hivyo amekanusha madai hayo na kusema kuwa alikwenda huko kutathmini maendeleo ya mchezo huo nchini Libya.

Lakini msemaji wa serikali ya Libya Moussa Ibrahim amesema kuwa Kanali Gaddafi hana mpango kama huo, na kwamba mustakhbali wa Libya utaamuliwa na walibya wenyewe.

Urusi na Umoja wa Afrika zimetoa wito kwa mzozo huo kumalizwa kwa njia ya kisiasa, ambapo mjini Berlin Kansela wa Ujerumani Angela aliunga mkono hatua ya umoja huo wa Afrika.

Petersberger Klimadialog Berlin Angela Merkel Klimaschutz
Kansela Angela MerkelPicha: dapd

´´Umoja wa Afrika mara zote umekuwa ukitaka kupatikana suluhisho kwa njia za kisiasa, na kwa njia njia hii tunashirikiana na umoja huo wa Afrika kwani nasi pia tuna mtizamo kama huo´´

Wakati huo huo maandalizi yanaendelea kwa ajili ya mkutano wa kimataifa utaoijadili Libya mkutano ambao umepangwa kufanyika mjini Istanbul Uturuki, Ijumaa ya wiki ijayo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters/ZPR

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman