1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wateka Bangui, Rais Bozize atoroka

24 Machi 2013

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize Jumapili (24.03.2013) amekimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Congo baada ya vikosi vya waasi kuutwaa mji mkuu wa Bangui.Waasi walikuwa wameapa kumpindua Rais Bozize.

https://p.dw.com/p/183PE
Waasi Afrika ya Kati.
Waasi Afrika ya Kati.Picha: AFP/Getty Images

Msemaji wa ofisi ya rais Gaston Mackouzangba amekaririwa akisema "Waasi wanaudhibiti mji huo. Natumai hakutakuwepo ulipizaji visasi." Imeripotiwa kwamba kulikuwepo na milio ya risasi na miripuko katika mji mkuu huo. Tokea Ijumaa miji kadhaa imekuwa ikitekwa na waasi baada ya makubaliano kati ya waasi hao na serikali kusambaratika. Makundi mbali mbali ya upinzani yanaunda muungano wa waasi unaojulikana kama Seleka.

Harakati mpya za waasi

Waasi hao kwanza waliuteka mji wa Bossangoa ambao uko magharibi mwa nchi hiyo na baadae waliuteka mji wa Damara ambapo ndipo ulipo mpaka wa kusitisha mapigano kati ya waasi na vikosi vya serikali kwa mujibu wa makubaliano ya amani. Waasi hao wa Seleka haukukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka jeshi la serikali ambalo halikufunzwa vyema na halina silaha za kutosha.

Waasi wa Seleka katika maeneo ya vijijini kilomita chache kutoka Damara.
Waasi wa Seleka katika maeneo ya vijijini kilomita chache kutoka Damara.Picha: AFP/Getty Images

Afisa wa wizara ya mambo ya nje amekiambia kituo cha televisheni cha Al Jazeera kwamba waasi pia wanadhibiti vituo vya televisheni na radio vya taifa. Awali mshauri mmoja wa rais aliyekataa kutajwa jina lake amesema Bozize amevuka mto Oubangi na kuingia Congo Jumapili asubuhi wakati waasi walipokuwa wakielekea kwenye kasri la rais.

Muungano wa waasi wa Seleka ulianzisha tena uhasama wiki hii katika nchi hiyo na kuapa kumuangusha Bozize ambaye wanamtuhumu kwa kuvunja makubaliano ya amani yaliofikiwa hapo mwezi wa Januari kuwajumuisha wapiganaji wake katika jeshi la taifa.

Wasifu wa Bozize

Bozize alinyakuwa madaraka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2003. Mwanajeshi huyo mkimya mwenye umri wa miaka 66 anayejulikana zaidi kwa jina la "Boz" alipatiwa mafunzo yake ya kijeshi na mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa. Historia yake imegubikwa miongoni mwa mambo mengine na kuishi uhamishoni,kufungwa gerezani, kuteswa na kufanya majaribio ya mapinduzi.

Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.Picha: Getty Images

Baada ya Bozize na vikosi vyake kumpindua Ange- Felix Patasse hapo mwaka 2003 alibadili uamuzi wake wa kutogombania urais na kushinda uchaguzi wa rais hapo mwezi wa Mei mwaka 2005 kwa ahadi ya kuijenga upya nchi hiyo ya kimaskini yenye utajiri wa madini. Alichaguliwa tena kuwa rais hapo mwaka 2011.

Bozize alizaliwa tarehe 14 mwezi wa Oktoba mwaka 1946 nchini Gabon ambapo baba yake alikuwa mwanamgambo wa polisi chini ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Familia yake inatoka kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutoka kabila lenye watu wengi la Gbaya.Alifikia cheo cha Ugenerali akiwa na umri wa miaka 32.Wakati alipokuwa gerezani hapo mwaka 1990 aliteswa na aliponea chupuchupu kuuwawa.Inaelezwa kwamba Bozize hana haiba kubwa lakini anajitambulisha kuwa ni "mjenga nchi" na "mzalendo" wakati wakosaji wake wanasema utashi wake mkuu ni kukalia madaraka.

Mashambulizi ya Seleka

Ufaransa hapo Jumamosi imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura kuzungumzia mzozo huo ulioko katika koloni lake la zamani. Kufuatia mkutano huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetowa taarifa kwa vyombo vya habari ikiwaonya waasi kwamba watachukuliwa hatua kali kwa ukiukaji wowote wote ule wa haki za binaadamu katika maeneo wanayoyadhibiti.

Waasi na serikali waliposaini makubaliano ya amani mjini Libreville, Gabon Januari 11 2013.
Waasi na serikali waliposaini makubaliano ya amani mjini Libreville, Gabon Januari 11 2013.Picha: dapd

Waasi wa Seleka walianzisha mashambulizi dhidi ya serikali hapo mwezi wa Disemba mwaka jana na kudhibiti miji kadhaa kabla ya kuanza kuusogelea mji mkuu wa Bangui. Hali hiyo imeifanya Ufaransa, Marekani na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati kuteremsha vikosi vyao nchini humo. Waasi walimtuhumu Bozize kwa kukengeuka makubaliano ya amani ya mwaka 2007 na walidai ajiuzulu.

Hapo mwezi wa Februari waasi na serikali waliunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kusaini makubaliano ya amani huko Gabon. Chini ya makubaliano hayo Bozize alikuwa amepangiwa kumaliza kipindi chake cha urais hapo mwaka 2016.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ina utajiri wa madini wenye kujumuisha dhahabu,almasi na urani lakini inaendelea kuwa miongoni mwa nchi kumi maskini kabisa barani Afrika.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters/dpa

Mhariri: Bruce Amani