1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi watimuliwa Kharkiv,mashariki ya Ukraine

8 Aprili 2014

Polisi ya Ukraine imewatimuwa wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi huko Kharkiv, lakini wanamgambo wenzao wanaendelea kuyakalia majengo ya serikali huko Donetsk na Luhansk.

https://p.dw.com/p/1Bdx7
Vikosi maalum vya Ukraine vikiwatuimua waasi huko KharkivPicha: Reuters

Ukraine ikiungwa mkono na Marekani na nchi za Umoja wa ulaya inaituhumu Urusi kusimamia machafuko katika eneo la mashariki na kuyarejea yale yale yaliyopelekea Moscow kuimeza raasi ya Crimea mapema mwezi uliopita.Kama ilivyotokea Crimea,waandamanaji wameyavamia majengo ya serikali jumapili usiku huko Kharkiv,Donetsk na Luhansk wakishinikiza kura ya maoni iitishwe.

Urusi iliyokusanya wanajeshi wake karibu na mpaka wa Ukraine imewaonya viongozi wepya wa mjini Kiev wasipuuze madai ya majimbo yenye wakaazi wengi wanaozungumza kirusi-kusini mashariki ya Ukraine, kitovu cha viwanda na migodi ya Ukraine.

Waziri wa ndani wa Ukraine Arsene Avakov amesema wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wametimuliwa Kharkiv katika opereshini ya kupambana na magaidi iliyodumu dakika 18.

Waziri wa ndani Arsene Avakov amewatwika rais Vladimir Putin wa Urusi na rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovich jukumu la kukaliwa majengo hayo.

Urusi yalaumiwa kuwa nyuma ya uasi huo

Wanamgambo 70 waliokamatwa wanatuhumiwa na serikali ya Ukraine miongoni mwa mengineyo kuhusika na "harakati haramu za uasi,kuchochea fujo miongoni mwa jamii na kusababisha madhara kwa afya ya binaadam.

Ukraine Pro Russisch Protest Demonstranten Kharkiw
Waandamanaji wanaopigania kujiunga na Urusi mashariki ya UkrainePicha: Reuters

Hata hivyo waasi wanaendelea kuyashikilia majengo ya serikali huko Donatsk na Luhansk ambako walivunja jengo la idara ya upelelezi na kunyakuwa silaha.

Hali mashariki ya Ukraine inaangaliwa kwa jicho la wasi wasi na nchi za magharibi,zinazohofia Urusi isije ikaitumia biashara ya gesi kama turufu dhidi ya nchi za Umoja wa ulaya.

Marekani imeionya Urusi isiingilie kichini chini katika mzozo wa mashariki ya Ukraine ambako kwa maoni ya ikulu ya Marekani kuna ishara za kuaminika zinazoonyesha wanamgambo wa Ukraine wanalipwa ili wafanye fujo.

Msemaji wa uikulu ya Marekani Jay Carney anasema:"Ikiwa Urusi itaingia mashariki ya Ukraine naiwe moja kwa moja au kichini chini, hali ya mambo itazidi kuwa mbaya.Tunamtolea wito rais Putin na serikali yake waache kuchochea vurugu nchini Ukraine.Na tunawatahadharisha pia dhidi ya kuingilia kijeshi."

Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen nae pia ameionya Urusi akisema itafanya "kosa la kihistoria" ikiamua kuivamia tena Ukraine.

Ishara njema yaanza kuchomoza

Ishara pekee ya kutulia hali ya mambo,waziri Serguei Lavrov amethibitisha mkutano wa pande nne utakaozileta pamoja Urusi,Marekani,Ukraine na umoja wa ulaya huenda ukaitishwa haraka kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Ukraine.

Kerry und Lawrow in Paris
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov walipokutana Paris Marchi 30 iliyopitaPicha: picture alliance / AP Photo

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo