1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi watoa muda majeshi ya Gaddafi kujisalimisha

31 Agosti 2011

Wafuasi watiifu kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya,Muammar Gaddafi,wanakataa kuweka silaha zao chini na kujisalimisha kwa vikosi vilivyomlazimisha kuingia mafichoni.Hali hii inaleta kitisho cha mapigano zaidi nchini Libya.

https://p.dw.com/p/12QMH
Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi hadi sasa hajulikani aliko, amejificha na waasi wanadhani bado yuko nchini Libya.Picha: picture-alliance/dpa

Wafuasi watiifu kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi, wanakataa kuweka silaha zao chini na kujisalimisha kwa vikosi vya jeshi lililomlazimisha kuingia mafichoni. Hali hii inaleta kitisho cha kuzuka tena mapigano nchini Libya, wakati muda wa mwisho wa kufanya hivyo utakapomalizika baada ya sikukuu ya Idd el Fitr.

Baraza la taifa la mpito ambalo ndio linalotawala hivi sasa, likiwa na nia ya kuimarisha nguvu zake na kupunguza hali ngumu ya maisha baada ya miezi sita ya mapigano, lilipata kiasi cha dola bilioni 1.55 wakati kamati ya vikwazo ya umoja wa mataifa ilipotoa fedha ambazo zilikuwa zimezuiwa nchini Uingereza. Fedha hizo zilikuwa zimezuiwa kwa kuwa zilikuwa zinatumika na utawala wa Gaddafi. Viongozi wapya wamesema kuwa Libya huenda itaanza kuuza mafuta tena katika muda wa siku chache zijazo.

Katika mstari wa mbele wa mapambano kuelekea katika mji wa pwani wa Sirte ngome kuu ya Gaddafi, ambako mahasimu wake wanadhani huenda amejificha , wapiganaji wa baraza la taifa la mpito wamesitisha kwa muda mapigano , wakitekeleza amri ya kusitisha mapigano iliyotangazwa na viongozi wao hadi siku ya Jumamosi. Mwenyekiti wa baraza hilo Mustafa Abdel Jalil amesema.

"Iwapo majeshi ya Gaddafi hayatakubali pendekezo letu hadi Jumamosi, tutaukamata mji huo kwa mtutu wa bunduki".

Chef des Libyschen Übergangsrates Mustafa Abdul Dschalil
mwenyekiti wa baraza la taifa la mpito Mustafa Abdel Jalil, ametoa muda wa mwisho kwa wapiganaji watiifu kwa Gaddafi kuweka silaha zao chini.Picha: picture alliance / dpa

Ndege za jeshi la NATO zimekuwa zikiyashambulia majeshi ya Gaddafi karibu na mji wa Sirte na jumuiya hiyo imewahakikishia washirika wao wa Libya kuwa itaendelea na mashambulio ya kijeshi ya angani hadi mzozo huo utakapomalizika, kitu ambacho uongozi wa baraza la mpito unasema , mzozo huo utamalizika pale tu Gaddafi atakapokamatwa , akiwa hai ama ameuwawa.

Mustafa Abdel Jalil ambaye alikuwa waziri wa sheria wa Gaddafi , kabla ya kumkimbia mwaka huu, ameonya kuwa Muammar Gaddafi bado hajamalizika. Bado ni kitisho kwa Walibya pamoja na mapinduzi.

Waasi wa Libya huenda hawataki majeshi ya kigeni katika ardhi yao, lakini watahitaji msaada kutoka nje wakati wakielekea katika demokrasia ambayo hawajaifahamu, baada ya Muammar Gaddafi, amesema mratibu mkuu wa umoja wa mataifa Ian Martin. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa pia amependekeza kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada kwa Libya.

"Kuna umuhimu mkubwa kwa hivi sasa. Watu wa Libya wanahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa. Serikali ya mpito itatoa mapendekezo maalum katika siku chache zijazo. Nia yangu ni kuwapeleka wafanyakazi wa umoja wa mataifa nchini humo haraka iwezekanavyo".

UNO General Sekretär Ban Ki-moon
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameitaka jumuiya ya kimataifa kuisaidia LibyaPicha: picture alliance ZUMA Press

Katika uwanja uliopewa jina jipya la uwanja wa mashahidi mjini Tripoli, mamia ya watu walijikusanya kwa ajili ya sala ya asubuhi kwa ajili ya sherehe za Eid El Fitr ikiwa ni mwisho wa mfungo mtukufu wa Ramadhan, wakifurahia kuangushwa kwa Gaddafi. Ulinzi ulikuwa mkali katika uwanja huo ambapo Gaddafi alitarajia kuadhimisha miaka 42 ya mapinduzi yaliyomwingiza madarakani hapo Septemba mosi.

Mke wa Gaddafi na watoto wake watatu wamevuka mpaka na kuingia Algeria. Algeria ikihofia vuguvugu la mapinduzi ya umma katika mataifa ya Kiarabu kuwa huenda yakaingia nchini humo na wasi wasi kuwa Libya baada ya Gaddafi huenda ikawasaidia Waislamu wenye imani kali nchini humo, si miongoni mwa nchi chache za Afrika kulitambua baraza la taifa la mpito , NTC.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri : Josephat Charo