1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wauwa walinda amani 15 wa UN, Congo

Mohammed Khelef
9 Desemba 2017

Mashambulizi mabaya kabisa dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuwahi kutokezea ndani ya miaka 25 sasa, yameuwa wanajeshi 15 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 50 mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/2p3iR
Mission der Vereinten Nationen in der Demokratischen Republik Kongo MONUC
Picha: Getty Images/AFP/P. Moore

Mashambulizi hayo yaliyofanywa usiku wa kuamkia jana (Ijumaa, 8 Disemba) dhidi ya kambi ya wanajeshi hao iliyopo eneo la Kivu Kaskazini yanaripotiwa kuendelea kwa masaa kadhaa. Wengi wa walinda amani waliouawa ni kutoka Tanzania.

Rais John Magufuli wa Tanzania alielezea kufadhaishwa kwake na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za wanajeshi hao, sambamba na kuwaombea afya ya haraka majeruhi, watatu miongoni mwao wakiripotiwa kuwa na hali mbaya sana.

Kiasi cha wanajeshi watano wa Kongo nao pia waliuawa kwenye mashambulizi hayo, ambayo yanashukiwa kufanywa na kundi moja la waasi lenye nguvu kubwa kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Hadi sasa, walinda amani wengine watatu hawajuilikani walipo, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huku wengine zaidi ya 20 wakikimbizwa kwenye mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, kwa ajili ya matibabu.

Umoja wa Mataifa walaani

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Picha: picture-alliance/dpa/AP/B. Matthews

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alielezea "ghadhabu na kusikitishwa" kwake, huku akiyaita mashambulizi hayo kuwa "ni uhalifu wa kivita" na kuitolea wito serikali ya Kongo kufanya uchunguzi huru na wa haraka.  

Idara ya Mambo ya Afrika katika Wizara ya Nje ya Marekani ilisema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ya "kutisha."

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, Nick Birnback, alisema hayo yalikuwa mashambulizi mabaya kabisa dhidi ya walinda amani wa Umoja huo kuwahi kutokea tangu Juni 1993, pale wanajeshi 22 kutoka Pakistan walipouawa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Msemaji huyo aliyaita mashambulizi haya kuwa "yaliyokudhamiriwa na kupangwa vyema na kundi lenye silaha za kutosha."

Haifahamiki ni wakati gani hasa kikosi cha kuongeza nguvu kiliwasili baada ya mashambulizi, ulisema Umoja wa Mataifa.

Kivu Kaskazini kuna hali ngumu

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

"Hali kwenye eneo hilo ni ya mashaka sana, sana," alisema mkuu wa vikosi vyote vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix, aliyeongeza pia kuwa mashambulizi hayo yalitanguliwa na kuongezeka kwa harakati za makundi kadhaa yenye silaha mashariki mwa Kongo. Alisema mashambulizi hayo ni jibu kwa Umoja wa Mataifa ambao umeimarisha uwepo wake.

"Tunawakera, na hilo hawalipendi," alisema.

Kituo cha walinda amani kilichoshambuliwa kiko umbali wa kilomita 45 kutoka mji wa Beni, ambao umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na waasi wa kundi la ADF-Nalu, linaloshukiwa pia kufanya mashambulizi hayo ya Alhamis usiku. 

Kituo hicho ndicho kinachokaliwa na kikosi cha dharura cha Umoja wa Mataifa, ambacho kina ruhusa ya kukabiliana na makundi yenye silaha katika mkoa huo wenye utajiri wa madini. 

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo ndicho kikubwa na chenye gharama kubwa kabisa duniani, kikiwa na bajeti ya dola bilioni 1.14 na wanajeshi zaidi ya 16,500. 

Takribani walinda amani 300 wameshauawa tangu kikosi hicho kuwasili mwaka 1999, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo