1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waathirika wa mafuriko Pakistan waziba barabara

Kabogo Grace Patricia16 Agosti 2010

Hatua hiyo wameichukua kwa madai kuwa misaada inawafikia pole pole na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuongeza jitihada katika kuyashughulikia maafa hayo.

https://p.dw.com/p/OorZ
Waathirika wa mafuriko nchini Pakistan, wakigombea mfuko wa unga uliotolewa na wasamaria wema.Picha: AP

Mamia ya waathirika wa mafuriko nchini Pakistan leo wameziba barabara kuu wakiitaka serikali ya nchi hiyo kuongeza jitihada katika kulishughulikia janga hilo, huku mashirika ya misaada yakionya kuwa misaada inawafikia walengwa hao pole pole. Misaada hiyo ni pamoja na chakula, maji safi, madawa na makaazi ya muda.

Hasira miongoni mwa wananchi imeongezeka ikiwa ni takribani wiki ya tatu sasa tangu Pakistan ikumbwe na mafuriko hayo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 80 iliyopita na kuwaathiri zaidi ya watu milioni 170. Mamia ya vijiji nchini humo eneo ambalo lina ukubwa sawa na Italia vimefurika, barabara kuu zimebomolewa na maelfu ya wananchi waliopoteza makaazi yao wamelazimika kuweka mahema ya muda pembezoni mwa barabara wakingojea kupatiwa misaada, lakini misaada hiyo imekuwa ikichelewa kuwafikia. Hasira hiyo ya wananchi imeelezwa kuwa inaweza kuhatarisha utulivu wa kisiasa katika serikali hiyo isiyo maarufu ambayo inakabiliwa na wanamgambo.

Mkurugenzi wa shirika la misaada, Oxfam nchini Pakistan, Neva Khan amesema kuwa hali hiyo mbaya inayoendelea inatisha. Khan amesema kuwa wananchi wanahitaji kwa haraka maji safi ya kunywa, maeneo ya kujisaidia na vifaa vingine vya usafi, lakini msaada uliopo kwa sasa ni mdogo sana. Wananchi hao waliziba barabara kuu tano katika eneo la Sukkur, mji mkuu uliopo kusini mwa Pakistan katika jimbo la Sindh. Wanavijiji hao walitishia kuyavamia magari yatakayopita katika maeneo ya karibu.

Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa leo umeonya kuwa kiasi watoto milioni 3.5 wako katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza kutokana na maji machafu nchini Pakistan yanayosababishwa na mafuriko hayo. Mbali na mafuriko hayo kuwaathiri wananchi hao, pia yameharibu mazao, miondombinu, miji, vijiji na kuwaua watu wengine 1,600. Hatua hiyo imeusababisha Umoja wa Mataifa kutoa wito kwa wafadhali wa kimataifa kuongeza msaada wenye thamani ya dola milioni 460. Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinaadamu OCHA, Maurizo Giuliano, amesema ana wasi wasi kuwa vifo vinaweza vikaongezeka Pakistan iwapo misaada hiyo haitapatikana.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Nick Clegg, amesema kuwa amekosoa jinsi jumuiya ya kimataifa inavyoyashughulikia maafa hao huko Pakistan, akisema kuwa baadhi ya nchi hawajajua ukubwa wake. Bwana Clegg ambaye amekaimu madaraka kutoka na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, David Cameron kuwa likizo, amesema wakati Uingereza imechukua hatua kubwa na madhubuti katika kuyashughulikia maafa hayo, mataifa mengine pia yanatakiwa kuongeza jitihada. Wito huo ameutoa wakati ambapo Kamati ya Majanga ya Dharura-DEC chombo chenye jumla ya mashirika 13 ya misaada ya nchini Uingereza hadi sasa kuchangisha Pauni milioni 15 kwa ajili ya maafa hayo nchini Pakistan. Serikali ya Uingereza kwa upande wake imetenga kiasi cha Pauni milioni 31.3 kwa ajili ya maafa hayo. Jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, aliyatembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo nchini Pakistan na kutoa wito wa kuongezwa misaada zaidi na pia alielezea jinsi alivyohuzunishwa na hali aliyokumbana nayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman