1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wacatalonia wapanga foleni kupiga kura ya maoni

Caro Robi
1 Oktoba 2017

Wacatalonia wamepanga foleni kupiga kura katika kura ya maoni iliyopigwa marufuku na serikali kuu ya Uhispania. Shirika la habari la Reuters limeripoti mamia wamejitokeza katika vituo kadhaa vya kupiga kura Barcelona.

https://p.dw.com/p/2l2Bn
Spanien Referendum Katalonien Demonstration
Picha: picture-alliance/Zumapress/M. Oesterle

Kura hiyo ya maoni ambayo Wacatalonia wanataka kujitenga na kujitawala imetajwa na serikali kuu ya Uhispania kuwa kinyume na sheria na haijabainika wazi iwapo vituo vya kupigia kura vitaruhusiwa kufunguliwa kama ilivyopangwa.

Msafara wa malori karibu 100 ya polisi, yameondoka kutoka bandari ya Barcelona leo asubuhi. Maelfu ya polisi wametumwa mjini humo kutoka kila pembe ya Uhispania kuzuia kura hiyo ya maoni kutofanyika.

Mahakama za Uhispania ziliamua kuwa kura hiyo ya kujitenga kwa jimbo la Catalonia inakiuka katiba na serikali kuu imejaribu kutumia kila mbinu za kisheria kuzuia isifanyike. Kufuatia maagizo ya majaji na waendesha mashitaka, polisi imechukua karatasi za kupigia kura, kuwakamata waandaaji wakuu wa kura hiyo na kuifunga mitandao ambayo inatetea kura hiyo yenye utata.

Kura ya maoni yawagawanya Wahispania

Hata hivyo, Kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont amesisitiza utawala wake umeweka mikakati yote kuhakikisha kuwa kura hiyo inafanyika. Jimbo hilo la Catalonia lililo kaskazini mashariki mwa Uhispania lenye utajiri mkubwa lina idadi ya watu milioni 7.5. Utajiri wa jimbo hilo ni mkubwa kuliko wa Ureno.

Katalonien Carles Puigdemont
Kiongozi wa Catalonia Carles PuigdemontPicha: Reuters/A.Gea

Uchunguzi wa utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa eneo hilo limegawanyika vibaya kuhusu kutangaza uhuru lakini wengi wa Wacatalonia wanataka kufikia maamuzi kuhusu hatma ya jimbo lao kupitia kura ya maoni.

Serikali kuu ya Uhispania imesema haitatambua matokeo yoyote ya kura hiyo na pia Jumuiya ya kimataifa inatarajiwa kutoyatambua.

Wizara ya mambo ya ndani imesema siku ya Jumamosi, polisi ilifunga takriban vituo 2,315 vya kupigia kura katika jimbo hilo. Hata hivyo vituo 160 vilikaliwa na watu wakiwemo, walimu, wazazi, wanafunzi na wanaharakati ambao wamepania kuhakikisha vinasalia wazi ili watu waweze kupiga kura.

Duru kutoka serikali ya jimbo la Catalonia imesema upigaji kura utafanyika katika maeneo mengine mbali na shule kama katika vituo vya afya na katika makazi ya wazee waliostaafu. Wakulima na wazima moto pia wameahidi kuvilinda vituo vya kupigia kura.

Puigdemont amewatolea wito wapiga kura watakaoshiriki katika kura hiyo ya maoni ya leo Jumapili kudumisha amani. Maelfu ya watu waliandamana kote nchini Uhispania Jumamosi ikiwemo mjini Barcelona wakitaka Uhispania kusalia kuwa taifa moja.

Serikali ya kihafidhina ya Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy imeshutumiwa na baadhi ya waandamanaji hao kuwa haijaushughulikia ipasavyo mzozo wa Catalonia isipokuwa tu kujirudia mara kwa mara kuwa ni kinyume na katiba.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: John Juma