1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachuuzi wahamishwa soko jipya la Muthurwa nchini Kenya

P.Martin30 Aprili 2008

Wachuuzi wamehamishwa kutoka eneo kuu la biashara katikati ya mji mkuu wa Kenya Nairobi na kupelekwa soko jipya la Muthurwa lililotengwa kwa ajili ya wachuuzi.Je hatua hiyo imeathiri vipi biashara ya wachuuzi hao?

https://p.dw.com/p/DrVr
Ramani ya Kenya na mji mkuu Nairobi.Picha: AP GraphicsBank/DW

Jackson Gitonga ni mchuuzi mmojawapo aliehamishwa katika soko jipya la Muthurwa na hana malalamiko kwani biashara yake inaendelea kustawi.Yeye anasema, biashara yake iliathirika wakati wa machafuko ya hivi karibuni kufuatia uchaguzi wa Desemba mwaka jana kwani hakuweza kutoka nje kufanya biashara.Hapo ndio alipata hasara kwa mara ya kwanza tangu kuanzisha biashara ya kuuza viatu vilivyotumika hiyo miaka mitatu iliyopita.Hata hivyo hakuvunjika moyo kwani anaweza kuendesha maisha yake.

Lakini kwa miaka kadhaa wachuuzi wengi walipinga kuhamishwa,kwa hofu ya kuhatarisha biashara iliyo na mashaka tangu hapo mwanzo.Kwa mfano,Joel Maina anahisi kuwa biashara yake ilikuwa ikistawi zaidi alipokuwa CBD,yaani eneo la biashara katikati ya Nairobi. Mwanzoni alikataa kuhama kwa sababu kituo cha mabasi kwenye soko la Muthurwa kilikuwa bado kikijengwa na hivyo walikuwepo wateja wachache sana.

Hata hivyo,utaratibu wa kugawa nafasi za kufanyia biashara umezusha mabishano makali kwani alietangulia ndio aliepata sehemu ya biashara.Ghasia zilizuka kati ya wachuuzi na halmashauri ya jiji kuhusika na ugavi wa nafasi hizo za biashara.Wachuuzi wanataka nafasia zaidi katika soko la Muthurwa lililo kiasi ya kilomita moja na nusu kutoka CBD.Kwa mujibu wa halmashauri ya jiji la Nairobi,kuna hadi nafasi 8,000.Lakini hivi sasa,kuna zaidi ya wachuuzi 12,000 katika soko la Muthurwa.Ni dhahiri kuwa uhaba wa nafasi ni tatizo kubwa katika soko hilo.

Kwa mfano mchuuzi John Mwaura anaeuza peremende na vitu vingine vya mchanganyiko anasema,tangu alipomaliza shule ya sekondari miaka minane iliyopita,anafanya biashara ya uchuuzi na huitazama familia yake. Analalamika kuwa wanalazimishwa kuhamia Muthurwa na hali hakuna nafasi za kuwapa.Je,atapata wapi pesa za kula?Au ndio aanze kuiba?

Kwa upande mwingine kuna tatizo la rushwa pia.Kwani watu wanaodai kuwa wachuuzi wanachukua hadi vibanda vinane na baadae huvikodisha kwa wengine.Mtindo huo unakwenda kinyume na azma halisi ya soko la Muthurwa. Kwani soko hilo lilipoanza kujengwa mwaka 2006,Musikari Kombo aliekuwa waziri wa serikali za mitaa alisema,soko hilo litakuwa kwa ajili ya wachuuzi tu na wala hakutokuwepo madalali.Huku wachuuzi wakihangaika kutenzua matatizo yao,wenye biashara mjini Nairobi wana furaha kubwa.Kwani muda mrefu walikuwa wakilalamika jinsi walivyokerwa na wachuuzi.Kwa maoni yao,serikali imefanya vizuri kuwahamisha wachuuzii kutoka sehemu za kati za mjini Nairobi.