1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WADA: Vipimo kuchunguzwa upya

6 Mei 2016

Shirika la kimataifa la kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni – WADA linasema kuwa vipimo vilivyofanywa na maabara tatu ambazo zilisimamishwa kazi karibuni vitachunguzwa upya

https://p.dw.com/p/1IjIh
Symbolbild Doping Labor
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Coffrini

WADA katika mwezi uliopita ilisimamisha kwa muda maabara zisizofanya kazi sawasawa nchini China, Ureno na Afrika Kusini, na kuvuruga mchakato wa vipimo kabla ya michezo ya Olimpiki mjini Rio mwezi Agosti.

Rais wa WADA Craig Reedie anasema wanariasha safi “hawastahili kuwa na wasiwasi” kuwa vipimo vimeathirika au vimo hatarini”.

Anasema maabara nyingine 31 zilizoidhinishwa na WADA kote duniani zitavishughulikia vipimo zaidi, “hivyo kuhakikisha kuwa hakuna mianya” katika upimaji. WADA haijafafanua namna maabara hizo zilishindwa katika majukumu yake, lakini iliashiria kuwa vifaa vilivyopitwa na wakati ni mojawapo ya sababu.

Kiprop awinda dhahabu Rio

Iikiwa imesalia chini ya miezi mitatu kabla ya tamasha la Olimpiki kuanza nchini Brazil, bingwa mara tatu wa duniani na Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Mkenya Asbel Kiprop, ni miongoni mwa wanariadha wa Kenya wanaojiandaa kuiwakilisha Kenya katika Olimpiki.

Mwanariadha huyo amewatawala kwa muda mrefu mbio hizo lakini alipoulizwa ikiwa anahisi shinikizo lolote hivi ndivyo alivyojibu "Wakati mwingine, shinikizo hukusaidia kabisa, kila mmoja anakuangalia…hebu mwangalie Rudisha anavyofanya katika kila mashindano anayoshiriki. Lakini kuwa na shinikizo hili katika mbio za mita 1,500, tuna wanariadha wazuri, hakuna kizuizi kikubwa kati yangu na Silas Kiplagat, au kati ya namba moja na namba nne katika mbio hizi. Hivyo ni changamoto kubwa, ndo maana unahitaji kujiandaa kwa mbio za kasi au za polepole.

Kiprop tayari ametangaza kuwa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki Rio, ndilo lengo lake mwaka huu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu