1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademocrat Marekani washinda viti muhimu

6 Novemba 2013

Chama cha Democrat nchini Marekani kimeshinda uchaguzi katika majimbo ya New York na Virginia, ambayo yalikuwa yakiongozwa na warepublican. Chama cha Republican kilishinda uchaguzi mwingine katika jimbo la New Jersey.

https://p.dw.com/p/1ACt4
Meya mpya wa New York Bill de Blasio na familia yake wakisherehekea ushindi.
Meya mpya wa New York Bill de Blasio na familia yake wakisherehekea ushindi.Picha: Reuters

Uchaguzi huo wa jana ni wa kwanza mkubwa kufanyika nchini Marekani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2012, ambao rais Barack Obama alishinda na kupata muhula wa pili madarakani.

Katika jiji kubwa zaidi nchini humo, New York, mwanasiasa mwenye msimamo wa kiliberali Bill de Blasio alishinda uchaguzi kwa tiketi ya chama cha Democrat, akimshinda kwa mbali mpinzani wake Joe Lhota wa chama cha Republican, na kuwa meya wa kwanza mdemocrat kupewa ufunguo wa jumba la meya wa New York tangu mwaka 1989.

Uchaguzi mwingine muhimu ulikuwa katika jimbo la Virginia ambalo kawaida ni ngome ya chama cha Republican lakini baada ya ushindani mkali. Terry McAuliffe alitangazwa mshindi katika kinyang'anyiro cha ugavana, dhidi ya Ken Cuccineli wa chama cha Republican aliyekuwa mwanasheria mkuu wa jimbo hilo.

New Jersey yabakia kwa warepublican

Chama cha Republican hakikuambulia patupu. Mgombea wake wa ugavana katika jimbo la New Jersey, Chris Christie alimshinda kwa kishindo mpinzani wake wa chama cha Democrat Barbara Buono.

Chama cha Democrat pia kilipata ushindi katika mji uliofilisika wa Detroit, na katika mji wa Boston.

Meya mpya wa New York Bill de Blasio na familia yake
Meya mpya wa New York Bill de Blasio na familia yakePicha: Getty Images

Na katika jimbo la Virginia, mfumo wa wakazi wake uliokuwa wa wanavijiji wenye mrengo wa kihafidhina unabadilika na kuwa wa miji yenye maoni ya kiliberali, uchaguzi huu pia ulikuwa kipimo cha namna kura itakavyopigwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.

Muundo wa wakazi wa jimbo hilo umebadilishwa na kuongezeka kwa wakazi ambao ni wafanyakazi wa serrikali na wanajeshi.

Kitisho kwa mahafidhina

Ushindi wa Chris Christie katika jimbo la New Jersey, sambamba na kushindwa kwa mwenzake wa jimbo la Virginia Ken Cuccineli, unaweza kuimarisha dhana kwamba pengine chama cha Republican kinapaswa kuwatenga wagombea wake wenye misimamo mikali ya kihafidhina.

Kushindwa kwa Cuccineli hasa kunachukuliwa kama kipigo kikubwa kwa kundi la Tea Party lenye mrengo mkali wa kulia katika chama cha Republican, ambalo katika uchaguzi wa mwaka 2010 lilifanikiwa kuwaingiza wajumbe wengi katika bunge mjini Washington.

Rais Barack Obama aliwapigia simu washindi wa chama cha Democrat na kuwapongeza. Ushindi huo, hususan katika jiji la New York unatazamwa kama wezani wa maoni ya umma huku uchaguzi wa bunge wa katikati mwa muhula utakaofanyika mwaka 2014 ukibisha hodi.

Hata hivyo wapo wachambuzi wasiokubaliana na maoni hayo, wakisema yaliyotokea katika majimbo ya Virginia na New Jersey hayawezi kutabiri yatakayojiri katika uchaguzi wa wabunge na magavana katika sehemu nyingine za nchi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/Reuters

Mhariri:Hamidou Oummilkheir