1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademokrat wampigia debe Hillary Clinton

26 Julai 2016

Vigogo miongoni mwa vigogo wa chama cha Democratic cha Marekani, Michelle Obama na Bernie Sanders wameshangiriwa walipohutubia mkutano mkuu wa chama chao na kusema Hillary Clinton anastahiki kuwa rais wa Marekani .

https://p.dw.com/p/1JVvT
Bernie Sanders alipotangaza kumuunga mkono Hillary Clinton Julai 12 iliyopita,huko PortsmouthPicha: Getty Images/D. McCollester

Katika wakati ambapo uchunguzi wa maoni ya umma unamtaja Donald Trump kumpita Hillary Clinton katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha rais wa Marekani,mke wa rais wa sasa wa Marekani Michelle Obama amewasisimua umati wa wafuasi wa Democrats waliohudhuria mkutano mkuu wa Philadelphia alipokosoa tabia ya Trump na kusifu dhamira ya kumkabidhi madaraka mwanamke awe rais wa Marekani kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.

Wito wa Michelle Obama ulikuwa wa kuleta suluhu na wa dhati na ulipokelewa vyema na umati wa watu waliohudhuria kikao cha ufunguzi cha mkutano mkuu huo wa siku nne. Baada ya kumsifu na kuzungumzia uwezo na sio rangi wala kabila Michelle Obama amesema kwa jazba kwa nini anamuunga mkono HIllary Clinton

"Kwasababu ya Hillary Clinton,binti zangu na watoto wetu wote, wanaume kwa wanawake,hivi sasa wanaamini mwanamke anaweza kuwa rais wa Marekani."

Kikao cha ufunguzi wa mkutano huo mkuu kilihanikizwa na sauti za wafuasi wa Bernie Sanders waliokuwa wakizomea kila wakati ambapo jina la Hillary Clinton lilikuwa likitajwa. Sauti hizo zilisita Michelle Obama na Bernie Sanders walipohutubia.

USA Wahlen Philadelphia Michelle Obama
Michelle Obama akihutubia mkutano mkuu wa Democrats huko PhiladelphiaPicha: Reuters/M. Kauzlarich

Mpinzani huyo wa Clinton katika chaguzi za mchujo amechagua pia kushadidia umoja na sio mtengano na kusifu mkondo wa mageuzi waliouanzisha pamoja na mashabiki wake. Bernie Sanders pia anasema Hiollary Clinton ndie kiongozi anaefaa kuiongoza Marekani .Anahoji:"Tunahitaji uongozi utakaowaleta pamoja wananchi wetu na kutufanya tuwe na nguvu zaidi na sio uongozi unaowatusi watu wenye asili ya Latin Amerika,waislam,wanawake,wamarekani weusi na wazee waliopigana vita na kutugawa. Kutokana na yote hayo,mdadisi yoyote mwenye kupima atatamka tu kwamba Hillary Clinton anastahiki kuwa rais mpya wa Marekani."

FBI kuchunguza tuhuma za kufichuliwa nyaraka za siri za chama cha Democrats

Mkutano mkuu wa chama cha Democrats umegubikwa na kisa cha kufichuliwa nyaraka za siri mtandaoni zinazoonyesha jinsi baadhi ya vigogo wa chama hicho walivyokuwa wakimfuja Bernie Sanders na washauri wake. Viongozi wa Chama cha Democratic wanaamini Urusi ilikuwa nyuma ya kufichuliwa nyaraka hizo zilizochapishwa katika mtandao wa Wikileaks. Urusi imekanusha tuhuma hizo. Shirika la upelelezi la Marekani linachunguza madai hayo.

USA Debbie Wasserman Schultz
Mwenyekiti wa Democrats ,Debbie Wassermann Schultz amelazimika kujiuzulu kutokana na kisa cha kufichuliwa nyaraka za siri na kuchapishwa mtandaoniPicha: picture-alliance/dpa/J. Behnken

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga