1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waichangia Syria dola bilioni 2.4

Admin.WagnerD15 Januari 2014

Wafadhili wanaokutana nchini Kuwait wameahidi kutoa kiasi cha dola bilioni 2.4 katika msaada wa kibinaadamu kwa waathrika wa vita nchini Syria, ambao mkuu wa umoja huo amesema nusu yao wanahitaji msaada wa dharura.

https://p.dw.com/p/1Ar0m
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa kuichangia Syria.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa kuichangia Syria.Picha: Reuters

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mgogoro huo umerudisha maendeleo yaliyopatikana nchini Syria kwa miaka 35 nyuma, huku nusu ya raia wake wakiishi katika hali ya umaskini. Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-Moon, alisema katika kilele cha mkutano huo kuwa zaidi ya dola bilioni 2.4 ziliahidiwa. Lakini ni asilimia 75 tu ya ahadi ya dola bilioni 1.5 zilizoahidiwa katika mkutano kama wa leo mwaka uliyopita zilizoufikia Umoja wa Mataifa.

Waziri John Kerry akizungumza jambo na waziri wa mambo ya kigeni wa Qatar, Khalid al-Attiyah.
Waziri John Kerry akizungumza jambo na waziri wa mambo ya kigeni wa Qatar, Khalid al-Attiyah.Picha: Reuters

Kuwait yaongoza michango

Kiongozi wa Kuwait Amir Sheikh Sabah al-Ahmed al-Sabah, aliahidi kiasi cha dola milioni 500 katika msaada mpya, wakati Marekani ilitangaza kutoa kiasi cha dola milioni 380. Qatar na Saudi Arabia zimeahidi dola milioni 60 kila mmoja, huku mataifa ya Umoja wa Ulaya ukiahidi jumla ya dola milioni 753. Uingereza iliahidi dola milioni 165, na Norway milioni 75.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema sehemu ya msaada walioutoa itawasaidia Wasyria kukabiliana haraka na baridi mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa, na hasa ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kutengeneza joto na kupikia, ununuzi wa mablanketi na mahitaji mengine muhimu kwa mamia ya maelf ya watu.

Umoja wa Mataifa ulitoa ombi la jumla ya dola za Marekani bilioni 6.5 kwa ajili ya watu wa Syria, kiasi ambacho ni zaidi ya mara nne ya dola bilioni 1.5 zilizoahidiwa katika mkutano kama huo mwaka uliyopita. Fedha hizo zilitumika ndani ya Syria na mataifa ya jirani kutoa chakula, madawa, maji ya kunywa na makaazi. Mchango mkubwa zaidi umetoka kwa mataifa ya Kiarabu ambayo yanawasaidia waasi wa Syria wanaopambana kumuondoa rais Bashar al-Assad.

Pande zote zapuuza wajibu wao kimataifa

Mkuu wa shughuli za kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Valeria Amos alisema pande zote katika mgogoro huo zimepuuza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kiutu na haki za binaadamu.

Amos alisema karibu raia 245,000 wanaishi katika miji iliyozingirwa na wanakabiliwa na hali ngumu sana, ikiwemo uhaba wa chakula, na kusema mbinu hiyo imegeuzwa kuwa zana ya kivita, huku malefu ya watu wakizuwia katika maeneo yao bila kuwa na uwezo wa kupata mahitaji ya msingi.

Mwanamke mkimbizi wa Syria akiwa na mtoto wake.
Mwanamke mkimbizi wa Syria akiwa na mtoto wake.Picha: ZAC BAILLIE/AFP/Getty Images

Makundi ya upinzani yanaendelea kuizingira miji ya Nubul na Al-Zahraa mkoani Aleppo, wakati vikosi vya serikali vinaendelea kizingira miji ya Ghouta mashariki, Daraya na Moadamiyet al-Sham iliyoko Damascus vijijini, na kambi ya wakimbizi w aKipalestina ya Yarmuk karibu na mji mkuu, na mji wa zamani wa Homs.

Wafanyakazi wa misaada wameituhumu serikali kwa kuzuwia upelekaji wa misaada hiyo kwa maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani, na kuwatishia kuwafukuza ikiwa watakwepa vizuwizi ili kuwasaidia maelfu ya watu waliyobanwa. Serikali mjini Damascus inalaumu mashambulizi ya waasi kwa kuchelewesha misaada.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Mohammed Khelef