1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wa migodi ya dhahabu wagoma

4 Septemba 2013

Mgomo wa wafanyakazi wa migodi ya dhahabu nchini Afrika Kusini Jumatano (04.09.2013)umeingia siku yake ya pili wakati hakuna mazungumzo zaidi yaliyopangwa kufanyika kati ya vyama vya wafanyakazi wa migodi na waajiri.

https://p.dw.com/p/19bsY
Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi Afrika Kusini (NUM).
Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi Afrika Kusini (NUM).Picha: Reuters

Lesiba Seshoka msemaji wa Chama cha Wafanya kazi wa Migodi cha Taifa(NUM) amesema mgomo huo unaendelea na kwamba hawakualikwa kwa mazungumzo mapya kujadili madai yao.Chama hicho cha wafanyakazi ambacho huwakilisha wafanyakazi wote wa migodi wanaogoma kimetupilia mbali ripoti kwamba imepunguza madai yao ya ongezeko la mishahara kutoka asilimia 60 hadi kuwa asilimia 10 tu.

Seshoka amesema NUM haikukubali ongezeko la mshahara la asilimia 10 na kwamba jambo hilo sio kweli,madai yao yako pale pale lakini wako tayari kwa mazungumzo ya ongezeko la mshahara kupindukia kima hicho.Waajiri wako tayari kutoaa ongezeko la mshahara la asilimia 6.5.

Maelfu ya wafanyakazi wa migodi ya dhahabu hapo Jumanne (03.09.2013) walianza mgomo baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya mshahara na kutishia kusababisha hasara ya mamilioni ya dola kutokana na kukosekana kwa uzalishaji katika sekta hiyo iliokumbwa na matatizo nchini Afrika Kusini.

Ulinzi waimarishwa migodini

Hali katika mgodi wa dhahabu wa Doornkop ulioko kilomita 30 magharibi ya Johannesburg hapo Septemba Nne 2013.
Hali katika mgodi wa dhahabu wa Doornkop ulioko kilomita 30 magharibi ya Johannesburg hapo Septemba Nne 2013.Picha: Reuters

Inakadiriwa kwamba wafanyakazi wa migodi 14,000 wameweka chini nyenzo zao za kazi katika mji wa migodi wa Carletonville kusini mwa Johannesburg. Usalama kwenye migodi ya eneo hilo umeimarishwa ambapo walinzi wa kibinafsi wenye silaha wamewekwa milangoni. Senyen'ge zimezungushwa kwenye lango kuu la mojawapo ya migodi ya kampuni ya dhahabu ya Anglogold Ashanti.Migodi yote saba isipokuwa mmoja tu inatarajiwa kuathiriwa na mgomo huo ikiwemo ya kampuni ya AngloGold Ashanti ,Harmony na Sibanye Gold.

Msemaji wa kike wa sekta ya dhahabu nchini Afrika Kusini Charmane Russel ameliambia shirika la habari la AFP kwamba sekta hiyo inatazamiwa kupata hasara ya kilo 761 za uzalishaji wa dhahabu kila siku zenye thamani ya dola milioni 34.

Mbuyiseli Hiban katibu wa NUM katika mkoa wa mji wa migodi wa Carlestonville amesema wafanyakazi zaidi wanatazamiwa kujiunga na mgomo huo leo hii.Amesema huo ni mgomo halali na wafanyakazi hawaogopi kupoteza ajira zao kama ilivyokuwa huku nyuma.

Mazingira magumu ya kazi

Wafanyakazi wa migodi hiyo ya dhahabu wanadai ongezeko la mshahara la kati ya asilimia 60 hadi 100 na kushutumu mishara ya juu wanayopokea wakurugenzi wakuu wa makampuni ya migodi wakati wafanyakazi wa migodi wakiishi katika umaskini mkubwa katika nchi hiyo yenye pengo kubwa kati ya maskini na matajiri.

Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya dhahabu ya Harmony huko Carletonville kusini mwa Johannesburg.
Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya dhahabu ya Harmony huko Carletonville kusini mwa Johannesburg.Picha: ap

Mgomo huo utaongeza shinikizo kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika ambapo takriban wafanyakazi 75,000 katika sekta ya ujenzi na viwanda vya magari wako katika mgomo.Kwa miongo kadhaa Afrika Kusini ilikuwa mzalishaji mkuu wa dhahabu duniani lakini fungu lake la uzalishaji limepungua kutoka asilimia 68 hapo mwaka 1970 hadi kufikia asilimia sita ya uzalishaji wa jumla wa dhahabu duniani hapo mwaka jana.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Josephat Charo