1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa wapiga kura kulichagua bunge

Sekione Kitojo
11 Juni 2017

Wapiga kura nchini Ufaransa wanapiga kura leo Jumapili (11.06.2017) katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge wakati chama cha rais Emmanuel Macron kinaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kupata wingi wa wabunge.

https://p.dw.com/p/2eT8k
Frankreich | Wahlwerbung für die anstehende Prlamentswahl
Picha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Macron amekuwa  akiogelea  katika  bahari  ya  umaarufu  mwanzoni  mwa utawala  wake  katika  wiki  tano  tangu  alipomshinda  mgombea  wa  siasa kali  za  mrengo  wa  ulia Marine Le Pen  na  kuwa  rais  kijana  kuliko  wote katika  historia  ya  ufaransa, akilitangaza  baraza  lake  la  mawaziri  ambalo linavuka  mipaka  ya  mrengo  wa  kushoto  na  kuonesha  mvuto  katika mikutano  ya  kimataifa.

Frankreich | Wahlwerbung für die anstehende Parlamentswahl
Mabango ya wagombea uchaguzi wa bunge mjini ParisPicha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Chama chake cha  siasa  za  wastani cha  Republique en Marche (Republic on the Move, REM) ama Jamhuri  inayopiga  hatua, chama  ambacho alikiasisi  mwezi  Aprili, 2016  kama  jukwaa  lake  alilotumia  kuwania  urais, sasa  kinahitaji  wingi  wa  kutosha  katika  bunge  la  taifa  ili  kumuwezesha kufanya  mageuzi  aliyoahidi.

Uchunguzi  kadhaa  wa  maoni  ya  wapiga  kura  unakionesha chama  cha Macron  kwamba  kinaweza  kuchukua  karibu  asilimia  30 ya  kura katika uchaguzi  wa  leo , na  kukiweka  katika  nafasi  ya  mbele  kabisa  kuweza kupata  wingi wa  kutosha  katika  uchaguzi  wa  duru  ya  pili wiki  moja  ijayo. Hii  inaweza  kutafsiriwa kuwa  ni  viti 400 katika  bunge  lenye  viti 577. Chama  cha  REM tayari  kimepata  msukumo  baada  ya  wagombea  wake kuwa  wa  kwanza  katika  majimbo 10  kati  ya  11  ya  nje  ya  nchi ambayo yamepiga  kura  kabla  ya uchaguzi  wa  leo.

Frankreich Parlamentswahlen
Mpira kura akiweka kura yake katika sanduku la kupigia kura mjini ParisPicha: AP

Wanawake wengi wamejitokeza

Jumla  ya  wagombea  7,882  wanagombea  nchi  nzima  katika mchakato ambao unatarajiwa  kushuhudia  sura  mpya  zikiingia  bungeni, sio kwasababu  zaidi  ya  wabunge 200 hawagombei  tena  katika  uchaguzi  huu. Wastani  wa  umri  wa  wagombea  ni miaka  48.5 na  zaidi  ya  asilimia  42  ni wanawake.

Katika  bunge  lililopita  wanawake  walikuwa  na  uwakilishi  wa asilimia  26.9 wa  wabunge , ama  jumla  ya  wanawake 155  katika  bunge lenye  viti 577, hali  ambayo  kwa  wakati  huo  ni  kubwa.

Iwapo  hakuna  mgombea  atakayeshinda  zaidi  ya  asilimia  50 katika  duru ya  kwanza, wawili  ambao  wamepata  kura  nyingi  wanaingia  katika  duru  ya pili,  pamoja  na  mgombea  yeyote ambaye  atashinda  kuwa  kwa  zaidi  ya asilimia  12.5 za jumla  ya wapiga  kura  katika  majimbo ya  uchaguzi.

Frankreich | Wahlwerbung für die anstehende Parlamentswahl
Mabango ya wagombea viti vya ubunge mjini Paris Juni 11, 2017.Picha: Getty Images/AFP/C. Archambault

Vituo  vya  kupigia  kura  vilifunguliwa  tangu  majira  ya  saa mbili  asubuhi kwa  saa  za  Ulaya  ya  kati  na  vitafungwa  katika  miji  mikubwa  mnamo saa  mbili  usiku  kwa  saa  za  Ulaya  ya  kati. Zaidi  ya  polisi 50,000 watakuwa  katika  doria  nchini  humo  ambamo  bado  hali  ya  hatari inaendelea  kufuatia  wimbi  la  mashambulizi  ambayo  yamewauwa  zaidi  ya watu  230  tangu  mwaka  2015.

Ugaidi

Katika  tukio  la  mwisho , ambalo lilifanyika  Jumanne, mtu  mmoja  mwenye umri  wa  miaka 40 ambaye  alijiingiza  mwenyewe  katika  imani  za  itikadi kali  mzaliwa  wa  Algeria  alipigwa  risasi  na  kujeruhiwa  baada  ya kumshambulia  polisi  kwa  nyundo  nje  ya  kanisa la  mjini  Paris la  Notre Dame.

Akiwa  amedhoofika  baada  ya  kupata kura  chache  kupita  ilivyotarajiwa dhidi  ya  mshindi  wa  uchaguzi  nchini  Ufaransa  Emmanuel Macron,  Marine Le Pen wa  chama  cha  National Front  anataka  kujionesha  kuwa  chama chake  ndio  chama  kikuu  cha  upinzani  baada  ya  kupata  kura  milioni 10.7 katika  uchaguzi  wa  mwezi  Mei.

EU Parlamentswahl 25.05.2014 Marine Le Pen
Kiongozi wa chama cha National Fron Marine Le PenPicha: picture-alliance/dpa

Macron amewapiga  marufuku  wagombea  wote  kuwaajiri ndugu  zao  iwapo watachaguliwa  na  ni  lazima  wafanye kazi  za  ushauri  wakati  wakiwa wabunge.

Frankreich Parlamentswahlen - Francois Fillon
Francois Fillon baada ya kupiga kuraPicha: AP

Hatua  hiyo  inafuatia  kashfa  iliyoporomosha  fursa  ya  urais  kwa mgombea  wa  chama  cha  mrengo  wa  kulia  cha  Republican , Francois Fillon, ambaye  anakabiliwa  na  madai  ya  uhalifu  kwa  kumlipa  mkewe Penelope zaidi  ya  euro  900,000 akimuajiri  kama  msaidizi  wake  bungeni.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / dpae

Mhariri : Bruce Amani