1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa wapiga kura

Stumai George6 Mei 2012

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anaelekea kushindwa katika duru ya pili ya Uchaguzi wa Urais unaofanyika leo nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/14qgk
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: Reuters

Sarkozy anaweza kuwa Rais wa kwanza aliyepo madarakani kuondolewa baada ya muhula mmoja tu na kumfanya awe kiongozi wa 11 barani Ulaya kuondolewa  kutokana na mtikisiko wa uchumi na kumpa nafasi mpinzani wake Francois Hollande kuwa Rias wa kwanza Msoshalisti katika kipindi cha miaka 17 iliyopita.

Kutokana na hasira za wananchi baada ya Sarkozy kushindwa kuupatia ufumbuzi ukosefu wa ajira katika muhula wake wa miaka mitano, Hollande alikuwa mbele zaidi ya Sarkozy kwa alama katika ya nne na nane katika kura ya maoni juu ya uchaguzi huo ambao unaweza kuleta mabadiliko barani Ulaya.

Licha ya kupoteza alama kadhaa mbele ya mpinzani wake katika siku za mwisho za kamapeni, wasaidizi wa Mhafidhina Sarkozy wamekiri kuwa itakuwa ni maajabu kwa mshirika wao huyo kushinda duru hii ya uchaguzi na kuendelea na muhula wa pili wa utawala wake.

Watu wake wapoteza matumaini

"Yeye ni kama mkimbiaji, hawezi kukubali kushindwa hadi mwisho wa mbio lakini naweza kusema ana nafasi moja katika kila nafasi sita", Mmoja wa watu wa karibu wa Sarkozy aliliambia Shirika la Habari la Reuters muda mfupi kabla ya kufungwa kwa kampeni siku ya Ijumaa.

Naye mwanauchumi Dominique Barbet anasema kuwa uhakika wa matokeo mazuri ya kura kwa Sarkozy umeshuka na kuwa kiwango cha chini sana.

Hollande mwanasiasa maarufu amesimama imara kwa wiki kadhaa baada mwezi Januari kutangaza mpango wake wa kuzidisha kodi kwa matajiri ili kugharamia matumizi na kupunguza nakisi.

Francois Hollande Kiongozi wa Wasoshalisti
Francois Hollande Kiongozi wa WasoshalistiPicha: Reuters

Kutokana na mpango wake huo, Hollande anafaidika kwa kuungwa mkono na watu wanaompinga Sarkozy na namna anavyoshughulikia masuala ya uchumi.

Uchaguzi huu wa Ufaransa unafanana na ule wa Ugiriki ambao pia wapiga kura wanatarajia kuviadhibu vyama vikubwa vya siasa kutokana na mgogoro wa uchumi.

Mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel mwanauchumi Paul Krugman amekiambia kituo cha televisheni cha Reuters mjini New York kuwa wapiga kura sasa wamechoshwa na sera zisizofaulu.

Sarkozy ambaye katika mbio hizo za kuwania Urais kwa muhula wa pili alikuwa akijulikana kama Sungura na mpinzani wake Hollande aliitwa Kobe, alizinduwa kampeni zake mwishoni na kuanza kumwaga sera zake moja baada ya nyingine kupitia hotuba za nguvu ambazo ziligonga mwamba kwa wafuasi wa mrengo wa kulia huku akitarajia kuungwa mkono na watu wenye kipato cha chini alijikuta akibwagwa na watu hao na wakaelekea pande nyingine.

Dhamira yake ya kupambana na wageni nchini Ufaransa kufanya mabadiliko ya kisera, kupunguza kodi na ukosefu wa ajira havikuweza kuishusha nafasi ya mpinzani wake. Aliwashangaza wengi pia aliposhindwa kumdhibiti mshindani wake katia mjadala wa televisheni siku kadhaa zilizopita.

Katika mapigo mengine mawili ya siku za mwisho za kampeni, mshiriki mwengine aliyeshika nafasi ya tatu kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Aprili aliyepata asilimia 17.9 Mzalendo Marine Le Pen na Mshiriki mwengine mwenye siasa za mrengo wa kati Francois Bayrou aliyeibuka na asilimia 9.1  wote walikataa kumuunga mkono  Sarkozy.

Wakati Sarkozy akiitumia Jumamosi yake kwa faragha nyumbani kwake jijini Paris na mkewe mwanamitindo wa zamani Carla Bruni, Hollande na mshirika wake mwandishi wa habari Valerie Trierweiler walikuwa mitaani wakipeana mikono na watu wao wanaowaunga mkono huku wakisaini vitabu vya kumbukumbu katika maeneo ya vijijini.

Vituo vya kupigia kura viko wazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni kwa saa za nchi hiyo. Matokeo ya awali ya kura yatatangazwa mara tu baada ya kufungwa kwa kituo cha mwisho cha kupigia kura. Chombo cha habari kitakachotangaza matokeo kabla ya muda muafaka kitachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mwandishi: Stumai George/Reuters

Mhariri: Abdul Mtullya