1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagambia wapiga kura wakitaraji mabadiliko

6 Aprili 2017

Raia wa Gambia wanawapigia kura wabunge leo kwa mara ya kwanza tangu kuondoka madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Yahya Jammeh.

https://p.dw.com/p/2an4O
Gambia Präsident Adama Barrow | Amtsübernahme & Einweihungszeremonie in Bakau
Rais wa Gambia Adama BarrowPicha: Reuters/T. Gouegnon

Katika uchaguzi huu, vyama vingi vinatarajiwa kuingia bungeni baada ya miaka 22 ya utawala wa chama kimoja. Vyama kadhaa vya upinzani viliungana mwezi Disemba kumng'oa Jammeh uongozini na kumpa uongozi rais wa sasa Adama Barrow.

Kura hiyo ya wabunge inaashiria mwanzo mpya kwa taifa hilo dogo la Afrika Magharibi, ambalo viongozi wake wanasema wanataka kuliongoza katika hali ya maridhiano. Lakini wengine wana wasiwasi kwamba muungano huo wa upinzani uliompa madaraka Barrow, umeanza kuonesha nyufa.

Mizozo ya muungano huo ya ndani kwa ndani iliufanya ukavunjika, na hili linamaanisha kwamba vyama tisa ndivyo vitakavyoshiriki uchaguzi wa leo, kikiwemo chama cha Jammeh cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction na chama cha upinzani cha tangu jadi kilicho na nguvu kubwa cha United Democratic party.

Takriban Wagambia milioni moja ni wapiga kura

Lakini vyama hivi vitakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chama cha Gambia Democratic Congress, kinachoongozwa na vijana na ambacho kiongozi wake Mama Kandeh alipata nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais. Ikumbukwe chama hicho hakikuwa miongoni mwa vile vyama vya upinzani vilivyoungana kumuondoa Jammeh uongozini.

Gambia Wahlen
Wagambia wakisubiri kupiga kura nje ya kituo cha upigaji kuraPicha: picture alliance/AP Photo/J. Delay

Zaidi ya Wagambia 880,000, wametimiza vigezo vya kupiga kura huku vituo vya kupiga kura vikiwa vilifunguliwa saa mbili asubuhi na vitafungwa saa kumi na moja jioni. Musa Faye ni mkaazi wa mji mkuu wa nchi hiyo, wa Banjul na ana matumaini kwamba huenda mambo yakabadilika chini ya utawala mpya.

"Mambo yanaweza kubadilika, yanaweza kubadilika, kwasababu hata kisiasa, watu wako huru zaidi," alisema Faye, "unaweza kufanya kampeni zaidi na unajua una wagombea wengi wa kujitegemea na unaoweza kuwapigia kura pia ni wengi."

Viti 53 vya ubunge ndivyo vinavyowaniwa

Matokeo ya kwanza yanatarajiwa Alhamis jioni huku matokeo kamili yakiwa yameratibiwa kutolewa asubuhi ya Ijumaa.

Kuna viti 53 vya kuwaniwa katika bunge la Gambia, viti vitano zaidi ya vile vilivyokuwa mwaka 2012 na haya ni kwa mujibu wa tume huru ya uchaguzi nchini humo. Nafasi tano zaidi zitateuliwa na rais ili kuwepo na jumla ya viti 58.

Gambia Ex-Präsident Yahya Jammeh
Aliyekuwa dikteta wa Gambia Yahya JammehPicha: Reuters/C. G. Rawlins

Umoja wa Afrika, Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS pamoja na Umoja wa Ulaya, wametuma waangalizi kushuhudia wapiga kura wanavyoshiriki zoezi hilo. Mwangalizi mkuu wa Umoja wa Ulaya ambaye pia ni mbunge wa Jamhuri ya Czech, Miroslav Poche, ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa tume huru ya uchaguzi nchini Gambia, ilionesha uthabiti wake kwa kusimama imara dhidi ya shinikizo kutoka kwa Jammeh aliposhindwa kwenye uchaguzi wa mwaka jana, na kisha kufungua kesi dhidi ya uamuzi wa tume hiyo.

Hii ndiyo mara ya kwanza kabisa EU kutuma ujumbe wa waangalizi katika uchaguzi nchini Gambia na imetoa usaidizi wa kifedha kwa maandalizi ya uchaguzi huo, katika wakati ambapo hazina za serikali ya nchi hiyo ni tupu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/APE

Mhariri: Daniel Gakuba