1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waganda waadhimisha miaka 50 ya Uhuru

MjahidA9 Oktoba 2012

Waganda wakusanyika pamoja katika Uwanja wa Kololo nchini humo, kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Uganda kutoka utawala wa kikoloni wa Uingereza

https://p.dw.com/p/16Mm9
Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: dapd

Hakuna siku ilioonesha umoja wa waganda na mshikamano na kujivunia kuwa raia wa Uganda kama siku hii ya leo, hivyo ndivyo baadhi ya waganda wanavyohisi siku ya leo Oktoba 9 mwaka wa 1962, ambapo ni miaka 50 tangu walipojinyakulia uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Usalama umeimarishwa katika Sherehe hizo kubwa zinazofanyika Uganda na kuongozwa na rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni. Sherehe hizo zinahudhuriwa pia na wakuu wa nchi kadhaa za kiafrika, wakiwemo rais wa Jamhuri ya Kiemokrasia ya Kongo Joseph Kabila, Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, na Paul Kagame wa Rwanda.

Kulingana na mwandishi wetu mjini Kampala, rais Yoweri Museveni alikuwa akitarajiwa kuhutubia wananchi ambapo wengi wanaamini kuwa ataeendelea kusisitiza waganda kuwa na uzalendo.

Rais wa zamani wa Uganda Idi Amin Dadah
Rais wa zamani wa Uganda Idi Amin DadahPicha: Getty Images

Kasisi wa kianglikana Luke Orombi ndiye aliyefungua sherehe kwa maombi akiitakia baraka tele, na kukemea mambo kama ukosefu wa kazi, rushwa, umaskini na siasa zisizokuwa na muelekeo mzuri katika nchi hiyo.Naye Mufti wa Uganda, Sheikh Shaban Mubajje aliliombea amani taifa hilo la Afrika mashariki .

Hata hivyo huku baadhi ya raia wa nchi hiyo wakisherehekea maadhimisho hayo kuna wale wasioona umuhimu wa miaka hiyo 50 ya Uhuru, wakisema hakuna chochote cha kujivunia kwa kuwa maskini wanaendelea kuwa maskini katika taifa hilo lililowahi kutajwa na Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchill kama lulu ya Afrika.

Kiongozi wa Upinzani Kizza Besigye
Kiongozi wa Upinzani Kizza BesigyePicha: MICHELE SIBILONI/AFP/Getty Images

Hata hivyo lulu hiyo imepoteza thamani yake. Baada ya utawala wa kikatili wa Milton Obote katika miaka ya 1966 hadi 1971, na kufuatiwa na utawala wa kidikteta wa Idi Amin Dadah, rais wa sasa Yoweri Museveni naye yuko madarakani kwa miaka 26, huku wadadisi wengi wakisiasa wakitathmini Uganda kama nchi isiokuwa na demokrasia, huku polisi wakitumiwa kuulinda utawala ulio madarakani kwa kuwanyanyasa na kuwakandamiza wapinzani.

Sherehe hizi za miaka 50 za uhuru wa Uganda zinafanyika wakati kiongozi wa upinzani Kizza Besigye akiwa katika kifungo cha nyumbani na kuzuiwa kuhudhuria. Serikali imedai kwamba huenda kiongozi huyo akavuruga amani katika maadhimisho hayo. Hata hivyo awali Besigye alinukuliwa akisema kuwa kamwe hawezi kuhudhuria sherehe hizo kwa kuwa hakuna chochote alichokiona katika miaka hayo hamsini ila ni mateso na ukandamizaji wa upinzani unaofanywa na serikali ya Museveni.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Mohammed Abul-Rahman