1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waganga na madaktari wapiga vita UKIMWI

P.Martin24 Oktoba 2007

Shirika la Umoja wa Mataifa-UNICEF- linaloshughulikia watoto duniani linaonya,Afrika Kusini inakabiliwa na hatari ya kushindwa vita dhidi ya UKIMWI.Kwa mujibu wa UNAIDS,kiasi ya watu milioni 5.5 nchini Afrika Kusini wameambukizwa na virusi vya UKIMWI.

https://p.dw.com/p/C7re

Tatizo kubwa linalokabiliwa na Afrika Kusini ni kuwa wagonjwa wengi wa UKIMWI wanaona aibu kwenda hospitali kupata matibabu.Sasa katika mji wa Cape Town,shirika moja la misaada liitwalo HOPE yaani matumaini,linajaribu njia pekee kuwafikia wagonjwa wenye UKIMWI-yaani kwa kuanzisha ushirikiano kati ya zahanati na waganga wa kienyeji nchini Afrika Kusini.Hata shirika la Kijerumani linalotoa misaada kupambana na UKIMWI, linatazamia kuunga mkono jitahada hizo mpya.

Waganga wa kienyeji yaani Sangoma,hutumia miti shamba na mizimwi ya vizazi vya kale.Wananchi wengi wa Afrika Kusini huwaamini waganga hao kuliko madaktari wa kisasa.Kwa hivyo,katika mwaka 2001,kiongozi wa HOPE mjini Cape Town,bwana Stefan Hippler aliamua kuwajumuisha waganga katika matibabu ya wagonjwa wa UKIMWI.

Mmojawapo wa waganga tisa wanaoshirikiana na madaktari wa HOPE,ni Profesa Sobantu Kubukeli. Yeye ni Rais wa Jumuiya ya Waganga wa Kienyeji na Wataalamu wa Mitishamba,mjini Cape Town.Kwa maoni yake,tofauti kubwa iliyopo ni njia ya kutibu. Anaeleza hivi:

„Madaktari wa nchi za magharibi,daima hutafuta bakteria.Kwa mfano,mtu atakapokuwa na kidonda kwenye kidole,daktari atashughulika kutafuta bakteria tu.Lakini sisi waganga wa kienyeji, tunatibu mwili mzima kiakili,kiroho na kimwili.“

Licha ya kutofautiana katika njia za kutibu, Wasangoma yaani waganga wa kienyeji na madaktari wa kisasa,wametafuta njia ya kufanya kazi kwa pamoja.Kwa mfano,mgonjwa anaekwenda kwa mganga na mganga huyo huhisi kuwa mgonjwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI,basi humshauri kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi zaidi na baadae hupatiwa dawa zinazozuia virusi hivyo kuzaliana.

Mganga Sobantu Kubukeli amevutiwa na utaratibu huo akiamini,hiyo ni njia ya kupeana mawazo ya ujuzi wao.Kwani waganga wa kienyeji wanaoshiriki katika mradi wa HOPE,wamejifunza kutambua ishara za ugonjwa wa UKIMWI na iwapo mgonjwa huyo, anahitaji kupatiwa dawa haraka.Muhimu zaidi ni kuwa wagonjwa,huwaamini waganga kuliko madaktari wa kisasa na hivyo ni rahisi kuwashawishi kwenda hospitali kwa matibabu.

Shirika la Kijerumani linalosaidia kupiga vita UKIMWI,limetiwa moyo na mafanikio ya mradi wa HOPE na hivyo limeamua kuuunga mkono mradi huo.