1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagiriki bado washindwa kuunda serikali

MjahidA12 Mei 2012

Kiongozi wa chama cha kisoshalisti cha PASOK, nchini Ugiriki Evangelos Venizelos amekiri kwamba harakati zake za kuunda serikali zimeambulia patupu.

https://p.dw.com/p/14uCU
Kiongozi wa chama cha PASOK Evangelos Venizelos
Kiongozi wa chama cha PASOK Evangelos VenizelosPicha: dapd

Hali hii imeisongeza ugiriki katika hatua ya kurudiwa uchaguzi huku nchi hiyo ikikumbwa na mbinyo kutoka Umoja wa Ulaya juu ya kurekebisha hali yake ya kifedha.

Matamshi ya kiongozi huyo wa Kisoshalisti yamekuja wakati chama cha mrengo wa shoto cha Syriza kikikataa kuunga mkono muungano unaounga mkono mpango wa kubana matumizi.

Akizungumza na waandishi habari mjini Athens, Evangelos Venizelos amesema atamuarifu rais wa nchi hiyo Carolos Papoulias juu ya kushindwa kwake hii leo Jumamosi na kutarajia kwamba katika kikao hicho vyama vyote vitakubali kuwajibika. Rais Papoulias sasa ndiye atakuwa na kibarua kigumu cha kujaribu kuunda serikali mpya nchini humo.

Kiongozi wa chama cha Syriza Alexis Tsipras
Kiongozi wa chama cha Syriza Alexis TsiprasPicha: AP

Siasa za Ugiriki zinayumba baada ya wapiga kura kuviaibisha vyama vinavyounga mkono mpango wa kubana matumizi kukiwa hakuna nafasi yoyote ya kuunda serikali mpya jambo lililotarajiwa kuiweka nchi hiyo katika nafasi ya kupokea mkopo mwengine wa kunusuru uchumi wake na pia kutoiaga kanda ya sarafu ya Euro.

Kiongozi wa chama cha Syriza kinachopinga mpango huo wa kubana matumizi Alexis Tsipras amesema sio chama chake kilichofanya hivyo bali ni raia wote wa Ugiriki waliopiga kura siku ya jumapili. Chama cha Syriza kimekuwa cha pili kupinga mpango wa kubana matumizi.

Hata hivyo wanaharakati sasa wanasema kwa sasa kile kinachotabiriwa ni kuwa na uchaguzi kati kati ya mwezi wa Juni ambapo hatua hiyo inaangaliwa kama njia moja inayoweza kuharibu mipango ya Ugiriki ya kupambana na swala la kufufua uchumi wake huku chama cha Syriza kikiwa na nafasi ya kupata kura zaidi. Awali kura ya maoni ilionesha chama hicho huenda kikashinda kwa asilimia 27.7 ya kura, hii ikiwa ni alama 11 juu ikilinganishwa na uchaguzi uliofanyika siku ya jumapili.

Ujerumani yatoa Onyo kwa Ugiriki

Wakati huo huo , Ujerumani imeionya Ugiriki kuwa isitarajie fedha nyingine za msaada hadi pale itakapofanya mageuzi, kama ilivyokubaliana na washirika wa kimataifa. Ujerumani imesema pia kanda ya sarafu ya Euro itaweza kuhimili endapo Ugiriki itaamua kujitoa kwa ghafla kutoka uanachama wa kanda hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle,Picha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema pamoja na kwamba washirika wa Ugiriki wanataka kuisaidia nchi hiyo kutoka katika mkwamo, Ugiriki nayo inapaswa kuonyesha kuwa inataka kusaidiwa. Westerwelle amesema Ujerumani inapenda kuona nchi za kanda ya sarafu ya Euro zinaendeleza umoja wao, lakini akaongeza kuwa mustakabali wa Ugiriki ndani ya Umoja huo uko mikononi mwa Wagiriki wenyenwe.

Naye Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, amanukuliwa na gazeti la Rheinische Post leo akisema kuwa Ugiriki lazima itimize wajibu wake wa kifedha ili iendelee kuwemo ndani ya kanda hii inayotumía sarafu ya Euro yenye jumla ya wanachama 17.

Mwandishi Amina Abubakar/RTRE/AFPE

Mhariri Sekione Kitojo