1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea Urais nchini Marekani, wakutana katika mjadala wa mwisho.

Nyanza, Halima16 Oktoba 2008

Wagombea Urais nchini Marekani Seneta Barack Obama kupitia chama cha Democrat na John McCain wa Republican, wamekutana tena katika mjadala wao wa tatu na wa mwisho katika kampeni za Urais nchini humo mwaka 2008.

https://p.dw.com/p/Fb8D
wagombea wawili wa Urais nchini Marekani kupitia chama cha Democratic Seneta Barack Obama na mwenzie John McCain, ambao leo walikutana katika mjadala wa mwisho wa kampeni za uchaguzi.Picha: AP

Mjadala huo umefanyika ikiwa imebaki takriban wiki tatu kufanyika kwa uchaguzi nchini humo, Novemba 4.

Mjadala wao, umefanyika alfajiri ya leo kwa saa za Afrika mashariki, ambapo Seneta McCain alikuwa katika kazi kubwa ya kumdhibiti seneta Obama, ambaye kura za maoni zinaonesha kuwa aliongoza katika mdahalo huo na uliopita.

Katika mjadala huo uliuolenga masuala ya ndani, wagombea hao walinadi sera zao katika masuala mbalimbali hususan katika nyanja ya uchumi kama vile kodi, na pia masuala ya afya, elimu na jamii.

Wakizungumza katika mjadala huo uliooneshwa kupitia Televisheni John McCain na Barack Obama walikuwa wakitumia maneno makali katika kushambuliana juu ya kampeni ya uchaguzi wanazofanya.

Aidha wote wawili walikiri kuwa uchaguzi huo, ulikuwa mgumu na kwamba kila mmoja alikuwa akimlaumu mwenziye kugeuza mwelekeo wa kampeni, ambapo kwa upande wa seneta Barack Obama alisema asilimia 100 ya matangazo ya seneta MacCain katika televisheni yalikuwa yakimkashifu Obama, na kudai kuwa wapiga kura wangependa kusikia jinsi jinsi ya kushughulikia masuala ya uchumi.

Pia alilalamika kwamba mcCain alishindwa kuwazuia wafuasi wake wasiendelee kumchafulia jina ikiwa ni pamoja na kumuhusisha Obama kwa ugaidi

Kwa upande wake Seneta MacCain pamoja na mambo mengine amemtuhumu Seneta Obama kwa kutumia fedha nyingi katika kampeni, ambapo pia alimkosoa na sera yake ya kodi.

Mwisho wa mjadala huo wagombea hao wote wawili, walipata nafasi ya kujinadi kwa wapiga kura wao, ambapo Seneta John McCain wa Republican alianza kwa kusema ametumia muda wa maisha yake kulitumikia kwanza taifa hilo, na ni mlolongo wa ukoo wa McCain, ambao umetumikia nchi hiyo kwa muda mrefu wakati wa vita na amani, na anajivunia kwa utumishi wake.

Naye Seneta Barack Obama mgombea urais kupitia chama cha Democrat alifunga mjadala huo naye kwa kujinadi kwa kusema kuwa '' tunahitaji mabadiliko ya msingi nchini humu, na hicho ndicho ninachokitaka kukileta tunapaswa kuwekeza tena kwa wananchi wa Marekani na kupunguza kodi kwa watu wa tabaka la kati, katika huduma ya afya kwa wamarekani wote na chuoni kwa kijana yeyote anayetaka kwenda''.

Ni siku 19 tu, zimebaki ili Wamarekani waweze kuamua ni nani wanayemtaka kati ya John McCain na Barack Obama.