1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina washindwa uchaguzi wa Iran

29 Februari 2016

Rais Hassan Rouhani na kundi lake la wapenda mageuzi wapeta katika uchaguzi wa bunge na baraza la wataalamu wa kidini na kuiweka nchi hiyo katika nafasi nzuri ya kuelekea mageuzi

https://p.dw.com/p/1I41f
Kura za uchaguzi wa bunge zikihesabiwa
Kura za uchaguzi wa bunge zikihesabiwaPicha: Tasnim

((Viongozi wa kidini wenye msimamo mkali na wenye ushawishi mkubwa wanaelekea kupoteza viti vyao katika Baraza la Wataalamu wa Kidini kufuatia uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini Iran, huku wapenda mageuzi wakiongoza katika uchaguzi huo muhimu wa bunge na baraza hilo la maulamaa.

Mohammad Yazidi na Mohammad Taghi Mesbah-Yazdi, ni miongoni mwa wanasiasa muhimu kwenye kundi la wahafidhina wa Iran waliopigwa chini katika uchaguzi wa baraza la wataalamu wa kidini . Hao ni miongoni mwa wengi walioshindwa katika uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wataalamu wa Kidini na kisiasa uliofanyika siku ya Ijumaa yna ambao unaonesha kuwa Rais Hassan Rouhani na washirika wake wapenda mageuzi wanaungwa mkono na umma wa Iran.

Hadi sasa, wanamageuzi wamejinyakulia viti 15 kati ya 16 vya baraza hilo la wataalamu, matokeo ambayo yanadhihirisha kuangushwa kwa viongozi wa kidini wahafidhina wenye sauti nchini humo, viongozi hao ni pamoja na spika wa baraza hilo la kidini ambalo ni chombo muhimu nchini Iran.

Matokeo yaliyochapishwa leo na shirika la habari la Iran IRNA yanaonesha kwamba wahafidhina huenda vile vile wakapoteza wingi wao katika baraza hilo la kidini ambalo ndio chombo chenye mamlaka ya kumchagua kiongozi mkuu wa kidini nafasi ambayo ni muhimu sana katika maamuzi ya mustakabali wa maswala yote ya nchi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Khayatollah Ali Khamenei.

Wadadisi wa mambo wanahisi kwamba matokeo ya chaguzi hizo mbili yanatoa taswira ya kuwepo hatua muhimu ya mageuzi kwa iran na pia inaonesha ni kwa jinsi gani wairan walivyokuwa na imani na serikali ya Rouhani pamoja na sera zake kuelekea nchi za Magharibi. Uchaguzi huo ni wa kwanza kuwahi kufanyika tangu Rouhani alipotia saini makubaliano na nchi zenye nguvu duniani Julai mwaka jana kuhusiana na mpango wa Nuklia wa nchi hiyo mpango uliosababisha Iran kulegezewa vikwazo vya kiuchumi.

Rais Hassan Rouhani
Rais Hassan RouhaniPicha: Reuters/R. Homavandi/TIMA

Mohammed Yazdi mwenyekiti wa baraza hilo la wataalamu ameshindwa katika uchaguzi pamoja na mwenzake Mohammad Taghi Mesbah Yazdi ambaye akionekana kuwa mtu aliyemshawishi sana rais wa zamani mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmed Nejad.Kiongozi pekee wa kidini mwenye msimamo mkali aliyepita kwenye uchaguzi huo ni Ahmad Jannati.

Rais wa zamani Akbar Hashemi Rafsanjani na Hassan Rouhani wamejinyakulia viti katika kinya'ng'anyiro hicho. Kwa mantiki hiyo ushawishi wa viongozi wenye msimamo mkali umeonesha kupungua wakati wapenda mageuzi wakichukua nafasi kubwa ikiwemo pia kushinda viti vyote 30 vya ubunge Tehran.Hata hivyo matokeo kamili ya chaguzi zote mbili yanatarajiwa kutangazwa baadae leo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef