1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 50 walitupwa baharini Yemen

John Juma
10 Agosti 2017

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limesema mhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu aliwatupa zaidi ya wahamiaji 120 ndani ya bahari siku ya Jumatano wakati walipokaribia fukwe za Yemen.

https://p.dw.com/p/2hz4I
Flüchtlinge im Boot
Picha: Picture-alliance/dpa/E. Morenatti/AP

Wahamiaji 50 kutoka Somalia na Ethiopia walizamishwa baharini kwa makusudi wakati msafirishaji haramu wa binadamu alipowatupa baharini karibu na fukwe za Yemen. Hayo yamesemwa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa ni hali ya kushangaza na kinyume cha utu.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo la kimataifa la Uhamiaji IOM, wafanyakazi wake waligundua makaburi 29 ya wahamiaji katika ufuo wa Shabwa. Maiti za wahamiaji hao zilizikwa na wenzao ambao walinusurika.

Wahamiaji wengine hawajulikani waliko

Kulingana na IOM, mhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu aliwazamisha zaidi ya wahamiaji 120 ndani ya bahari siku ya Jumatano wakati walipokaribia fukwe za Yemen. IOM imeongeza kuwa wahamiaji wengine 22 hawajapatikana, na kwamba umri wa wastani wa wahamiaji hao umekadiriwa kuwa miaka 16.

Wahamiaji eneo la Harad-Yemen. (Picha ya maktaba)
Wahamiaji eneo la Harad-Yemen. (Picha ya maktaba)Picha: DW/Alsoofi

Laurent de Boeck ambaye ni mkuu wa ujumbe wa IOM nchini Yemen amesema, "Walionusurika waliwaambia wafanyakazi wetu kuwa, msafirishaji haramu wa binadamu aliwasukuma kwa nguvu kutoka kwenye boti kutumbukia baharini, pale alipowaona watu kama maafisa karibu na ufuo.

Pia walisema kuwa msafirishaji huyo amesharudi Somalia kuendeleza biashara yake haramu ya kuchukua wahamiaji wengine zaidi kuwaleta Yemen kupitia njia hiyohiyo."

IOM: Dhiki kubwa inawakumba wahamiaji

Wafanyakazi wa IOM wamewapa misaada wahamiaji 27 walionusurika na kubakia ufuoni hapo wakati wenzao wengine waliondoka kwenda zao. De Boeck amesema dhiki inayowakumba wahamiaji katika njia hiyo ni kubwa hasa wakati wa msimu wa upepo katika bahari Hindi.

Njia ya bahari kati ya pembe ya Afrika na Yemen imetumika sana na wahamiaji wanaotaka kufika katika nchi za Ghuba zenye utajiri wa mafuta. Hiyo ni licha ya machafuko ambayo yanaendelea nchini Yemen. De Boeck amesema kuwa vijana wengi huwalipa wasafirishaji haramu wa wanadamu kwa matumaini yasiyokuwepo ya mustakabali mwema.

Wahamiaji wa Ethiopia wakisubiri kusafirishwa Yemen. (Picha ya maktaba)
Wahamiaji wa Ethiopia wakisubiri kusafirishwa Yemen. (Picha ya maktaba)Picha: A. Ohanesian

Kulingana na takwimu za IOM, takriban wahamiaji 55,000 wametoka katika nchi za Pembe ya Afrika kuelekea Yemen tangu Januari mwaka huu, huku wengi wakitoka Somalia na Ethiopia. Theluthi moja ya wahamiaji hao wakikadiriwa kuwa wanawake.

Hatari ya vita vya Yemen

Licha ya mapigano yanayoendelea Yemen, wahamiaji Waafrika wameendelea kuwasili katika nchi hiyo isiyokuwa na utawala wa kitaifa unaoweza kuwazuia wasiendelee na safari yao. Wahamiaji wanajikuta katika hatari ya kudhulumiwa na magenge ya wasafirishaji haramu wa binadamu, ambao wengi wanahusishwa na makundi yenye silaha yanayoshiriki katika vita vya Yemen.

Mnamo mwezi Machi, serikali ya Somalia ililaumu muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen kwa kushambulia boti na kuwaua wakimbizi 42 wa Somalia katika bahari karibu na ufuo wa Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya mashirika ya kimataifa yanayoangalia uhamiaji katika eneo hilo, zaidi ya wahamiaji 111, 500 waliwasili katika ufuo wa Yemen mwaka uliopita, hiyo ikiwa ni ongezeko kutoka wahamiaji 100,000 waliowasili nchini humo mwaka uliotangulia.

Mwandishi: John Juma/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga