1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji walioingia Macedonia kurudishwa Ugiriki

15 Machi 2016

Mamia ya wahamiaji wameondoka katika kambi ya muda nchini Ugiriki na kuingia Macedonia baada ya kukwepa uzio wa mpakani uliowekwa kuwazuwiya na Macedonia imesema itawarudisha Ugiriki wahamiaji hao.

https://p.dw.com/p/1IDHA
Wahamiaji wakivuka mto kuingia Macedonia. (14.03.2016).
Wahamiaji wakivuka mto kuingia Macedonia. (14.03.2016).Picha: Reuters/S. Nenov

Msemaji wa polisi ya Macedonia amesema mamia ya wahamiaji ambao wamevuka mpaka na kuingia Macedonia watarudishwa Ugiriki. Mpiga picha wa shirika la habari la Uingereza Reuters amesema idadi ya wahamiaji hao waliovuka mpaka na kuingia Macedonia inaweza kufikia 2,000.

Waandishi habari 30 akiwemo mpiha picha huyo wa Reuters ambao waliwafuata wahamiaji hao pia walikamatwa.

Maafisa wa Ugiriki wamesema vipeperushi vilisambazwa katika kambi ya wahamiaji ya Idomeni vikiwataka watu kujiunga katika msafara wa kuelekea Macedonia.

Msemaji wa serikali ya Ugiriki George Kyritis amesema wana vipeperushi vyenye kuonyesha hilo lilikuwa tukio lililoandaliwa na la hatari sana lenye kuhatarisha maisha.

Maelfu wakwama Idomeni

Takriban wahamiaji 12,000 wakiwemo maelfu ya watoto wamekwama Idomenia katika mji mkubwa wa mahema kaskazini mwa Ugiriki baada ya njia yao wanayoitumia kuingilia Umoja wa Ulaya kufungwa kufuatia Macedonia na mataifa mengine yalioko katika kile kinachojulikana kama njia ya Balkan kufunga mipaka yao.

Msafara wa wahamiaji kuelekea Macedonia ukitokea Idomeni ,Ugiriki (14.03.2016)
Msafara wa wahamiaji kuelekea Macedonia ukitokea Idomeni ,Ugiriki (14.03.2016)Picha: Getty Images/M. Cardy

Hapo jana zaidi ya wahamiaji 1,000 waliandamana kutoka kambi hiyo wakitafuta njia ya kukwepa uzio mbili za mpakani zilizojengwa na Macedonia kuwazuwiya wasiingie nchini humo.Kundi jengine la wahamiaji lilifuata baadae wengi wakitoka maeneo ya vita nchini Syria na Iraq.

Wahamiaji walitembea kwa miguu kwenye njia zilizojaa matope wakibeba mikoba mgongoni na watoto mabegani.

Walipofika kwenye mto waliweka kamba hadi upande wa pili ambapo walivuka kwa kukamatana na walipofika kwenye eneo la milima upande wa pili wa mpaka walikamatwa na wanajeshi wa Macedonia na kuwapakia kwenye magari ya kiijeshi ambapo serikali imesema inafanya mipango ya kuwarudisha Ugiriki.

Makubaliano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya

Kuvuka kwa wahamiaji hao kumeliweka tena suala hilo la wahamiaji hadharani siku chache kabla ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki kukutana tena kukamilisha makubaliano yenye kukusudia kuwazuwiya wahamiaji nchini Uturuki kuingia Ulaya kupitia Ugiriki.

Griechenland Mazedonien Flüchtlinge bei Idomeni
Msafara wa wahamiaji kuelekea Macedonia ukitokea Idomeni ,Ugiriki (14.03.2016)Picha: Getty Images/M. Cardy

Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk Jumanne ameondoka kuelekea Cyprus na Uturuki katika juhudi za kukamilisha makubaliano ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kudhibiti wimbi la wakimbizi barani Ulaya.

Rais huyo wa Umoja wa Ulaya atakuwa mwenyeji wa mkutano mpya wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Ugiriki mwishoni mwa juma mjini Brussels.Kwa mujibu wa rasimu ya makubaliano hayo Umoja wa Ulaya umekubali kumpatia makaazi mapya mkimbizi mmoja wa Syria kutoka makambi ya Uturuki kwa kila kwa kila mkimbizi wa Syria aliyepokelewa na Uturuki kutoka visiwa vya Ugiriki.

Wakati huo huo shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limeyataka mataifa ya magharibi kuzisaidia nchi jirani na Syria zilizoelemewa na wakimbizi kuwapokea angalau wakimbizi 480,000 katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/Reuters/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman