1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa mafuriko walalamika kwa kukosa chakula

Josephat Charo7 Agosti 2007

Wahanga wa mafuriko kusini mwa Asia wamelalamika kuwa misaada bado haijawafikia, huku wabunge wa maeneo yaliyoathiriwa pamoja na maafisa wa serikali wakiripotiwa kuiba vyakula vya waathirika wa mafuriko hayo.

https://p.dw.com/p/CHjr
Wahanga wa mafuriko nchini Bangladesh
Wahanga wa mafuriko nchini BangladeshPicha: AP

Watu takriban 487 walikufa kutokana na kuumwa na nyoka, njaa au kutokana na magonjwa yanayosambazwa kupitia maji tangu mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea kusini mwa Asia. Wengine walikufa maji, kupigwa na vitu vilivyokuwa vikisombwa na maji na wengine kutokana na umeme.

Maelfu ya wahanga wa mafuriko hayo wameachwa bila makao katika eneo lililoathiriwa zaidi na mafuriko katika jimbo la Bihar, mashariki mwa India, siku kumi baada ya kile ambacho maafisa na wakaazi wamekieleza kuwa mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika historia.

Polisi wamesema wamefaulu kuokoa maiti 13 za watu waliokufa maji kwenye mto wa Ganges wakati mashua zilizokuwa zimebeba idadi kubwa ya watu kupita kiasi zilipopinduka kwenye mkoa wa Bihar. Watu wengine 50 hawajulikani waliko na ajali zaidi zimeripotiwa kutokea katika eneo hilo.

Rupesh Kunar, mkaazi wa kijiji kilichofunikwa na maji mkoani Bihar amesema hawajaona helikopta yoyote wala mashua ya serikali ikiwapeleka chakula tangu mafuriko yalipoanza siku 15 zilizopita.

Msemaji wa shirika la misaada la Oxfam katika eneo hilo, Aditi Kapoor, amesema wanajaribu kuwasaidia wahanga wa mafuriko.

´Shirika la Oxfam linaongeza juhudi za kuzisaidia familia elfu 50 ambazo zina watu laki mbili unusu kwa kuwapa misaada ikiwa ni pamoja na maji safi ya kunywa, kushughulikia usafi wao, chakula na makaazi ya muda.´

Bi Kapoor pia ameileza hali katika eneo hilo kuwa mbaya. ´Hali ni mbaya sana. Kwa hiyo watu wanajaribu kutafuta mahala pa kukaa mahala popote wanapoweza katika vilima. Na ingawa serikali inawaangushia vyakula, bado havitoshi.´

Hata hivyo kiongozi wa operesheni ya kutoa misaada jimboni Bihar, Meja Manoj Kumar Srivastava, amesema wameidhibiti hali na kufaulu kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kwa kuwaangushia vyakula wahanga wa mafuriko kutumia helikopta.

Kwa kuwa mafuriko husababisha magonjwa, shirika la Oxfam linaamini kuwa maji safi ya kunywa na kushughulikia mahitaji ya afya ya jamii kunaweza kuyaokoa maisha ya wengi.

´Hili ndilo jambo linalofanywa na Oxfam na kuishawishi serikali ilishughulikie eneo hili. Ni mapema kusema ikiwa kitu chochote kitafanyika. Kufikia sasa bado hatujasikia kuzuka kwa ugonjwa wowote lakini hofu ipo kila wakati na tunahitaji kujiandaa kukabiliana nayo.´

Maji yameanza kupungua nchini Nepal lakini watabiri wa hali ya hewa wanasema kuna wasiwasi kwamba mvua zaidi huenda ikanyesha huko Assam baada ya kusita kwa siku nne.

Nchini Bangladesh maji yanateremeka kutoka wilaya za kaskazini kwenda katikati mwa nchi. Maafisa wa utabiri wa hali ya hewa wameonya kwamba mafuriko zaidi yanatarajiwa katika mji mkuu Dhaka ulio na wakaazi milioni 11.