1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa tetemeko wakimbia wakihofia mafuriko China.

Mohamed Dahman17 Mei 2008

Maelfu ya wahanga wa tetemeko kubwa la ardhi lililopiga nchini China wanayakimbia maeneo yalio karibu na kitovu cha tetemeko hilo kutokana na hofu ya kuzuka mafuriko kutoka mto uliozibwa na maporomoko ya ardhi.

https://p.dw.com/p/E1bQ
Wahanga wa tetemeko la ardhi lililopiga jimbo la Sichuan nchini China.Picha: AP

Wanajeshi wamekuwa wakiwabeba wazee kuowandoa kutoka mji wa Beichuan katikati ya jimbo la Sichuan wakati watu wengine walionusurika wamekumbatia watoto wakiwa kwenye barabara iliojaa magari na watu.

Polisi mmoja ameliambia shirika la bahari la AFP kwamba maafisa wa uokozi wanahofu kwamba maji kutoka mto huo uliojaa yanaweza kufurika mji huo.Awali shirika la habari la serikali Xinhua limesema ziwa katika mji wa Beichuan yumkini likafurika kingo zake bila ya kutaja sababu za kujaa kwa maji kwenye ziwa hilo.

Maafisa wanasema tetemeko hilo la ardhi la ukubwa wa kipimo cha saba nukta tisa limewapotezea makaazi takriban wahanga milioni tano.

Idadi ya vifo imethibitishwa kuwa imeongezeka na kufikia karibu watu 29,000 wakati wengine maelfu kwa maelfu hawajulikani walipo.

Rais Hu Jintao ambaye yuko kwenye jimbo hilo amewahimiza waokozi kuzidisha bidii ili kuokowa maisha ya watu zaidi kwa haraka kadri inavyowezekana.

Miongoni mwa watu waliookolewa wakiwa hai kutoka chini ya vifusi vya majengo yalioporomoka katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita ni mtaalii mmoja wa Kijerumani.