1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri juu ya siku ya wanawake duniani

Abdu Said Mtullya8 Machi 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. Wanahoji, kuwa siku moja haitoshi kuwatilia maanani akina mama duniani.Mwaka unazo siku zaidi ya 300.

https://p.dw.com/p/14HdE
Mwanaharakati wa Misri Mona Eltahawy
Mwanaharakati wa Misri Mona EltahawyPicha: dapd

Gazeti la "Schwarzwälder Bote" linasema, leo ni siku ya wanawake duniani na linatoa hongera kwa akina mama wapendwa. Lakini mhariri wa gazeti hilo anauliza hongera hizo ni juu ya nini? Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba siku ya leo ilizinduliwa ili kuyatafakari masuala ya usawa wa jinsia,kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na kuzitetea haki za akina mama. Lakini mhariri wa gazeti la "Schwarzwälder Bote" anasema malengo hayo yamepotoshwa na baadhi ya wanasiasa na kuifanya siku ya leo isiwe na maana kama jinsi inavyostahili.

Kinachotakiwa ili kuifanya siku ya leo iwe na maana ni kwa wakubwa wa kazi kuchukua hatua za kuwaendeleza akina mama kazini. Lakini anasema hayo yanapaswa kufanyika kila siku katika mwaka.Siku moja tu haitoshi.

Mhariri wa gazeti la "Leipziger Volkszeitung" anasema wanawake wanastahiki kupata zaidi, na siyo siku moja tu, ambapo dunia inawakumbuka. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba katika kuiadhimisha siku ya leo, viongozi wa nchi, mameneja na wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi wanatuma salamu za pongezi kwa wanawake. Lakini wanawake wanastahili,zaidi ,na siyo salamu za pongezi tu.

Kwa mfano chama cha kijani nchini Ujerumani kimewasilisha ombi la kuleta usawa wa mishahara kwa akina mama. Chama hicho kimechukua hatua sahihi. Kwa sababu wanawake wanastahiki kupata zaidi ,kuliko siku moja tu ya kutiliwa maanani. Kwa hiyo badala ya siku ya leo tu,yaani tarehe 8 mwezi Machi, wanawake wanastahili kutiliwa maanani katika siku zote 365 za mwaka.

Mhariri wa "Mitteldeutsche Zeitung" anawalaumu wanasiasa wa Ujerumani kwa kuruhusu sheria zinazowakandamiza wanawake. Mhariri huyo anaeleza kwamba akina mama aghalabu huchagua kazi katika sekta ya huduma kwa sababu kazi katika sekta hiyo zinawafurahisha, ingawa wanalipwa kidogo.Kwao haidhuru. Lakini sasa mtindo wa maonevu umezuka katika sekta hiyo nchini Ujerumani.

Kwa mfano wanawake wanalipwa Euro 400 tu kwa mwezi.Na wengine wanapewa mikataba ya kazi za muda kama vibarua. Ni katika hayo ambapo waajiri wanawadhulumu wanawake hao.Lakini hayo yamewezekana kutokana na sheria zilizopitishwa na wanasiasa. Kwa hiyo sasa inapasa kujiuliza kwa makini iwapo wakati haujafika wa kuung'oa mzizi wa ustawi wa kazi hizo nchini Ujerumani.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Deutsche Zeitungen

Mhariri:Saumu Yusuf