1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti wazungumzia juu ya kupunguzwa kodi

Abdu Said Mtullya4 Julai 2011

Wahariri watoa maoni juu ya suala la kupunguza kodi nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/11obJ
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanauzungumzia mjadala juu ya kupunguza kodi na pia juu ya mgogoro wa Ugiriki.

Mhariri wa gazeti la Weser-Kurier anauunga mkono mjadala juu ya kupunguza kodi kwa kuwa una manufaa kwa wote . Sababu ni kwamba mfumo wa kodi wa sasa unasababisha utata mkubwa. Mhariri huyo pia anatilia maanani kwamba idadi ya watu wanaouona mfumo huo kuwa siyo wa haki inaoengezeka.

Gazeti la Neue Osnabrücker linasema mjadala juu ya kupunguza kodi ni wa manufaa kwa wananchi wote, lakini anauliza jee, vipi mpango huo utatekelezwa? Anaeleza kuwa suala la kupunguza kodi sasa limekuwa kaulimbiu ya serikali ya mseto ya Ujerumani. Lakini anasema hali haitakuwa nzuri kwa kuzungumzia tu mara kwa mara juu ya kupunguza kodi. Ni kweli kwamba pana sababu kwa nini watu,na hasa wenye vipato vya kati wapewe nafuu ya kodi.

Lakini chama cha waliberali, FDP kilichopendekeza mpango huo wa kupunguza kodi hakijasema vipi mpango huo unaweza kutekelezwa. Mhariri anaeleza kuwa, kutokana na kuongezeka deni la serikali , mpango wa kupunguza kodi utakuwa na maana ya kuliongeza deni la nchi ambalo sasa linakaribia Euro Trilioni 2.

Gazeti la Stuttgarter pia linatahadharisha juu ya mpango wa kupunguza kodi ,kwa kusema kuwa hesabu zinazotumika ni zile zinazotokana na ustawi uliopo sasa. Mhariri wa gazeti hilo anafafanua anasema hadi kufikia kipindi cha mapukutiko, vyama vinavyoiongoza serikali ya Ujerumani vinakusudia kuzungumzia juu ya kupunguza kodi ili kujiongezea kura katika uchaguzi wa mwaka 2013. Kwa sasa Ujerumani imefikia ustawi mzuri wa uchumi. Lakini hali ya uchumi haitakuwa hivyo wakati wote.

Gazeti la Neue Presse linazuungumzia mgogoro wa madeni ya Ugiriki na linahoji kwamba pana ulazima wa kubadili sheria ili kuepusha migogoro katika nchi zilizomo katika Umoja wa sarafu ya Euro. Mhariri wa gazeti hilo anasema Ili kuepusha migogoro, Umoja wa Ulaya unapaswa kufuatilia na kutoa ridhaa ya bajeti za nchi wanachama. Kwa upande mwingine utaratibu huo ungelikuwa na maana ya kujiingiza katika mambo ya mabunge ya kitaifa. Na hasa nchi tajiri kama Ujerumani hazipo tayari kuzibadili sheria.

Gazeti la Leipziger Volkszeitung pia linauzungumzia mgogoro wa Ugiriki, kwa kusema kwamba sasa maafa yaliyokuwa yanahofiwa kuifika nchi hiyo yameweza kuepushwa baada ya nchi hiyo kupatiwa mkopo wa dharura .Kwa kuzingatia hali ya ugegeu kwenye masoko ya fedha, kutolewa mkopo huo ni habari nzuri kwa Ugiriki.

Mwandishi/Mtullya abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman,Mohammed