1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wasema kauli tupu juu ya Israel hazitoshi.

Abdu Said Mtullya11 Machi 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kauli ya makamu wa rais wa Marekani Joe Biden ya kuilaani Israel na pia wanakumbuka mauaji ya Winnenden.

https://p.dw.com/p/MPbd
Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na waziri mkuu wa Israel Banjamin Netanyahu.Picha: AP

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden ameilaaniserikali ya Israel kwa uamuzi wake wa kuendeleza ujenzi wa makao ya walowezi mashariki mwa mji wa Jerusalem na hivyo kuhujumu juhudi za kuanzisha tena mazungumzo ya kuleta amani katika mashariki ya kati.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya hayo.Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mauaji yaliyotokea mwaka jana katika shule moja kusini mwa Ujerumani

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden ameilaani Serikali ya Israel kwa kuamua kujenga makaazi mapya 1600 ya walowezi.

Juu ya msimamo wa makamu huyo wa rais , bwana Biden mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anatilia maanani kwamba waziri wa mambo ya ndani wa Israel ameomba radhi juu ya uamuzi huo, uliotangazwa wakati bwana Biden anafanya ziara ya mashariki ya kati. Gazeti linasema Israel inataka dunia ikubali kwamba ilikuwa bahati mbaya uamuzi huo kutangazwa wakati wa ziara hiyo.

Lakini gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba watu huko Jerusalem wanasema uamuzi huo ulitangazwa kwa kudhamiria.

Gazeti la Westfälische Nachrichten linauliza jee ilichofanya Israel ni majikwezo au ni upumbavu ? Gazeti hilo linaeleza kwamba haitoshi kwa jumuiya ya kimataifa kutoa kauli kali.Ikiwa Israel inahujumu dhahiri, juhudi za kuleta amani, basi sasa inapasa kutafakari vikwazo madhubuti dhidi yake.


Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung ameghadhabishwa na anasema kuwa uamuzi wa Israel ni kitendo cha uchokozi-yaani bwana mdogo anajaribu kumfunga nira kaka mkubwa! Gazeti linasema hiyo ni sababu ya kutosha kwa rais Obama kumweleza wazi waziri mkuu wa Israel Netanyahu kwamba, licha ya kuwapo urafiki mahsusi baina ya Marekani na Israel, waziri mkuu huyo lazima atambue mipaka yake. Mhariri huyo anasema ,ikiwa rais Obama atasita kufanya hivyo,Isreal itapitisha maamuzi peke yake juu ya masuala mengine vile vile , kama juu ya Iran, na hilo linaweza kuleta hatari ya vita katika eneo lote la mashariki ya kati!

Siku kama ya leo mwaka mmoja uliopita kijana aliekuwa na umri wa miaka 17 aliingia ghafla shuleni na kuanza kufyatua risasi.Katika shambulio hilo,wanafunzi tisa na walimu watatu waliuawa. Maafa hayo yalitokea katika mji wa Winnenden kusini mwa Ujerumani.

Katika kuukumbuka mkasa huo gazeti la Main Post linasikitika kwa kusema kwamba kwa wote walioathirika na maafa hayo, tarehe ya leo haitaondoka maishani mwao.Na kwa wanasiasa walichofanya ni kutokea kwenye vyombo vya habari na kutoa matamko.

Mwaka mmoja baada ya kutokea maafa hayo, anasema mhariri wa gazeti hilo ,hali halisi ni kwamba sheria bado hazijabadilishwa vya kutosha juu ya umilikaji wa silaha!

Na mhariri wa gazeti la Trierischen Volksfreund anasema mageuzi ya sheria yaliyofanywa juu ya umilikaji wa silaha yamethibiti kuwa ni simba kibogoyo!

Mwandishi/ Mtullya

Mhariri/Hamidou Oummilkheir/

Abdu/Deutsche Zeitungen.