1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wasema kuteuliwa de Maizere ni uamuzi sahihi

Abdu Said Mtullya3 Machi 2011

Kuteuliwa Thomas de Maizere kuwa waziri mpya wa ulinzi, ni uamuzi wa busara na sahihi wanasema wahariri wa magazeti karibu yote ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/10SuS
Waziri mpya wa ulinzi Thomas de Maizere(Kulia)akipongezwa na Rais wa Ujerumani Christian Wulff.Picha: picture alliance/dpa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemteua Thomas de Maizere kuwa waziri wake mpya wa ulinzi baada ya waziri wa hapo awali zu Guttenberg kujiuzulu.

Wahariri wa magezeti wanatoa maoni yao juu ya uteuzi huo na karibu wote wanakubaliana kuwa uteuzi huo ni sahihi.

Gazeti la Lausitzer Rundschau linasema de Maizere, ambae hadi alipochaguliwa alikuwa waziri wa mambo ya ndani, ni mtu mwenye uwezo thabiti wa kazi. Na hicho ndicho hasa wanachokihitaji wanajeshi sasa.

Mhariri wa gazeti la Westfälische anakubaliana na maoni hayo kwa kusema kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amefanya uamuzi wa busara kwa kumteua mtu anaemwamini. Mhariri huyo anaeleza kwamba Thomas de Maizere ni mtu alieonyesha ustadi katika kuyatekeleza majukumu yake na pia ni mwanasiasa asiekuwa na dosari. Thomas de Maizere ndiye mtu ambaye Kansela Merkel hasa anamhitaji baada ya lawama kubwa zilizotolewa juu ya Kansela huyo kuhusu namna alivyoishughulikia kashfa ya zu Guttenberg.

Uamuzi wa Kansela Angela Merkel kumteua waziri wake wa mambo ya ndani kushika wadhifa wa ulinzi unaonyesha kuwa Kansela huyo hana muda wa kuingia katika maabara ya kisiasa na kufanya majaribio.Hayo anayasema mhariri wa gazeti la Sächsische.

Gazeti la Brauschweiger lina imani kwamba waziri mpya wa ulinzi de Maizere ni mtu mwafaka wa kuyatekeleza mageuzi katika jeshi la Ujerumani.Mhariri huyo anaeleza kuwa Thomas de Maizere ni mahiri sana, mchapa kazi na mwaminifu , ni mtu anaeyatimiza majukumu yake bila ya mayowe, awe waziri wa mambo ya ndani au waziri katika ofisi ya kansela. Uteuzi wake utakuwa na manufa makubwa kwa wanajeshi, kwa sababu sikio la Kansela lipo karibu na mwanasiasa huyo.

Na mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anasema mwanasiasa huyo kutoka chama cha CDU siyo kiraka cha kuzibia tairi lililopata pancha. Mwanasiasa huyo anahesabika kuwa miongoni mwa washirika wa ndani wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.


Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman