1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri waizungumzia Kenya, ushindi wa Merkel

Abdu Said Mtullya24 Septemba 2013

Wahariri wanazungumzia juu ya mgogoro wa nchini Kenya na mustakabal wa Ujerumani baada ya kufanyika uchaguzi mkuu

https://p.dw.com/p/19o1J
Wanajeshi wa Kenya wakipambana na magaidi
Wanajeshi wa Kenya wakipambana na magaidiPicha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani kwamba nchini Kenya majeshi ya usalama ya nchi hiyo bado yanaendelea kupambana na magaidi waliolivamia jengo la duka mjini Nairobi. Mhariri wa gazeti hilo anasema waislamu wenye itikadi kali wanazidi kuziyumbisha nchi za Afrika, lakini nchi za Afrika zitaendelea kupambana na watu hao.


Mhariri wa gazeti la "die tageszeitung" anatilia maanani kwamba jumuiya ya kimataifa sasa imeshazoea kuona nchi za Afrika, moja baada ya nyingine ikiyumbishwa na makundi ya magaidi. Kwanza ilikuwa Somalia na baadae ikafuatia Mali. Mhariri huyo anasema shambulio la magaidi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, linalenga shabaha moja; kuipeleka vita ndani ya Kenya.

Udugu wa Kiislamu

Gazeti la "Döbelner Anzeiger" linazungumzia juu ya kupigwa marufuku kwa chama cha Udugu wa Kiislamu nchini Misri. Na linasema hatua hiyo haitayatatua matatizo ya Misri- ni tabaini yake. Mfarakano wa nchi utazidi kuwa mkubwa. Misri inahitaji mdahalo na kwa hivyo kuwapiga marufuku Udugu wa Kiislamu maana yake ni kuiziba njia ya mdahalo.

Ushindi wa Angela Merkel

Gazeti la "Sächsiche" linauzungumzia ushindi wa Kansela Angela Merkel katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani. Lakini mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba,ushindi huo ulinywea siku moja tu baada ya kutangazwa.Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kwamba baada ya ushindi wa kihistoria sasa Merkel anakabiliwa na mtihani wa kuunda serikali. Lakini hawezi kuiunda serikali hiyo na chama cha kijani. Hana njia nyingine ila kuwakaribisha wapinzani wakuu, yaani chama cha Social Demokratik na kuunda mseto mkubwa.

Gazeti la "Westfalen-Blatt" linaiunga mkono hoja hiyo kwa kusema kuwa dalili zote zinaonyesha kwamba serikali ya mseto mkubwa itaundwa baina ya vyama vya kihafidhina, vya CDU ,CSU na chama cha Social Demokratik.Lakini wananchi wa Ujerumani wanasuburi kwa hamu kuona jinsi masuala ya kodi na mishahara ya kima cha chini yatakavyotatuliwa.

Naye mhariri wa "Westfälische Nachrichten", katika maoni yake anawasilisha ujumbe kwa chama cha Social Demokratik SPD kwamba chama hicho sasa kinapaswa kuacha kuzikaanga mbuyu za kampeni za uchaguzi. Mipango juu ya kuingia katika serikali ya mseto na Kansela Merkel ilishatayarishwa siku nyingi na mwenyekiti wa SPD na viongozi wenzake Naye mhariri wa "Kölner Stadt-Anzeiger"anasema kuunda serikali ya mseto baina ya pande zozote, kunahitaji moyo wa kuwa tayari kufikia mwafaka.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman