1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wammulika Barack Obama

Hamidou, Oumilkher5 Juni 2008

Eti kweli wamarekani watamchagua Obama awe rais wao?

https://p.dw.com/p/EE5n
Barack ObamaPicha: AP


Ushindi wa Senetor Obama katika kinyang'anyiro cha kuania tikiti ya chama cha Democratic kwa uchaguzi wa rais November ijayo nchini Marekani ndio mada iliyohanikiza magazeti hii leo.Gazeti la Die WELT linategea macho Marekani na kuandika:


"Obama ana wajib mkubwa,na Clinton jukumu kubwa pia linamsubiri.Kuna uvumi eti anapanga njama dhidi ya Obama ili ashindwe kwa namna ambayo atamng'owa madarakani McCain mwaka 2012 na kuingia yeye madarakani.Mbinu kama hizo zinaweza kukitia sumu chama chao.Wapiga kura milioni 18 wanaomuunga mkono Clinton hawana njia nyengine isipokua kumkubali Obama kama mgombea wa chama cha Democratic.Wakikataa ,watamfungulia mlango John McCain,mgombea pekee aliyewahi kuwa mfungwa wa vita,aapishwe kama rais wa Marekani.Na hilo pia litakua tukio la maana katika mwaka huu wa uchaguzi nchini Marekani."


Hayo ni maoni ya DIE WELT,gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG linaandika:


"Ushindi wa Obama ni jibu pia dhidi ya mtindo wa Washington unaofuatwa pia na akina Clinton.Hilarry alidharau hapo awali ,werevu wa mwanasiasa huyo mwenye asili ya kiafrika katika kuwahamasisha watu.Sasa bibi huyo mkakamavu anameza machungu ya ndoto ambayo haikutekelezeka."


Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika:


"Hatujui bado kama Barack Obama ndie atakaekua rais mpya wa Marekani.Kama wamarekani hatimae wataamua kweli kumpa kura zao senetor huyo mweusi na kijana, hakuna ajuaye.Tunajua tuu kwamba akichaguliwa Obama,ulimwengu mzima utafurahia.Hatutaishi katika ulimwengu mwengine lakini eti kwasababu Obama amechaguliwa kua rais.Marekani itaendeleya kupigania masilahi yake ya kimkakati sawa na itakavyoendela kujitia wahka.Ulimwengu hata hivyo utajipatia fursa ya kuwaangalia wamarekani kwa jicho jengine kabisa.Wataangaliwa kama mfano wa kuigizwa na sio mtihani,wataangaliwa kama rafiki badala ya mshirika."


Linaamini gazeti la Frankfurter Rundschau.Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE la mjini Erfurt lina wasi wasi upande huo:


"Hata nchini Ujerumani kuna watakaokunja uso Obama akichaguliwa.Senetor wa Illinois,ambae hajawahi hata kidogo kuingia katika uwanja wa kidiplomasia, anaiangalia nchi yake kama kitovu cha ulimwengu.Akitekeleza ahadi alizotoa,basi uchumi wa Marekani utazidi kuzorota.Malumbano makali zaidi yatashuhudiwa ikiwa vita vitaendelea kwa muda mrefu zaidi nchini Afghanistan na Iraq.Hapo ndipo miito ya kutaka wanajeshi wa shirikisho Bundeswehr wapelekwe ng'ambo itakapozidi makali mara dufu."


Gazeti la RHEINISCHE POST la mjini Düsseldorf linamulika makundi ya wapiga kura kutoka tabaka ya wafanyakari,wale wenye asili ya Latin Amerika na wanawake wa kizungu na kuandika:


"Hadi hivi punde hakufanikiwa Obama kuivutia jamii hiyo ya wapiga kura.Ndio maana kuna umuhimu mkubwa hivi sasa kwake kuwageukia na kuwatanabahisha wakinamama hiyo ikiwa njia bora zaidi ya kuwafikia wamarekani wa daraja ya wastani.Labda kwa kushirikiana pamoja na Hilary Clinton.Hawezi kuepukana na kushirikiana na bibi huyo japo ameshindwa.Wapiga kura milioni 18 wanamuunga mkono-idadi takriban sawa na ile ya wanaomuunga mkono Obama."