1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasema Marekani itavuruga sheria za kimataifa

Abdu Said Mtullya7 Machi 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani watoa maoni juu ya mvutano baina ya Israel na Iran na juu ya sera ya Marekani juu ya magaidi. Endapo itatekelezwa wanaoitwa magaidi na Marekani wanaweza kuuawa.

https://p.dw.com/p/14GN2
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Barack Obama
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Barack ObamaPicha: dapd

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kukaa kimya wakati Rais Assad anaigeuza nchi yake kuwa kizimba cha mateso na uwanja wa mauaji halaiki. Mhariri wa gazeti hilo anasema China, Urusi na katika sehemu zingine za dunia watu hawataki kuuona ukweli huo nchini Syria.

Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine"amekariri aliyoyasema mshairi maarufu wa enzi ya Uyunani Aischylos miaka 2500 iliyopita,kwamba, kinachokufa kwanza katika vita ni ukweli.

Gazeti la"Lübecker Nachrichten"leo linazungumzia juu ya mvutano baina ya Israel na Iran. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu anazinoa zana tayari, kwa kuishambulia Iran. Lakini mhariri huyo anatanabahisha kwa kueleza kwamba watawala wa Iran hawatanyamaza kimya ikiwa Israel itaishambulia mitambo ya nyuklia ya Iran. Madhara yake yatakuwa makubwa sana katika eneo lote la Mashariki ya Kati ambapo kwa sasa harakati za mapinduzi zinaendelea. Mhariri wa "Lübecker Nachrichten" anasisitiza kuwa Mashariki ya Kati haihitaji vita ambapo hapatakuwa na mshindi.

Gazeti la "Hessische/Niedersächsiche Allgemeine"linasema Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu hajali, iwapo watu wanamwona hana subira. Anachotaka ni kuishambulia Iran. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa kwa kadri mahandaki ya kuifichia mitambo ya nyuklia yanavyozidi kuwa marefu, vivyo ndivyo itakavyokuwa vigumu kwa shambulio la Israel kufanikiwa dhidi ya Iran. Na katika mazingira hayo Israel italazimika kuomba msaada wa Marekani. Ndiyo sababu gazeti linasema kwamba Waziri Mkuu Netanyahu anataka Israel iwe na uwezo wa kujiamulia sera zake yenyewe haraka.

Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linasema kila hatua ya kidiplomasia inapaswa kuchukuliwa ili kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia. Sababu ni kwamba vita baina ya Israel na Iran itakuwa na madhara yasiyoweza kupimika.

Gazeti la " Der neue Tag" linazungumzia juu ya mpango wa Marekani wa kuwaua inaowaita magaidi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujihami. Juu ya sera hiyo gazeti hilo linasema Marekani itakiuka haki za binadamu na itazivuruga sheria za kimataifa. Ikiwa kila nchi duniani itaifuata sera hiyo, basi kila serikali itakuwa na uhuru wa kuwaua wapinzani wake na kuwaita magaidi. Gazeti la "Der neue Tag" linasema tukumbuke kwamba mnamo miaka ya 80 Iran iliitekeleza sera kama hiyo na nchi za magharibi zilipiga kelele kubwa!

Mwandishi:Mtullya Abdu

Herkunft:Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo