1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasema nyota zimekaa kombo kwa Merkel na Sarkozy

Abdu Said Mtullya24 Aprili 2012

Wahariri leo wanazumngumzia juu ya kusambaratika serikali ya Uholanzi na juu ya mshikimano baina ya Rais Sarkozy na Kansela Merkel baada ya kufanyika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/14k2t
Merkel na Sarkozy
Merkel na SarkozyPicha: dapd

Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anasema kuanguka kwa serikali ya Uholanzi maana yake ni kutetereka nguzo muhimu ya Umoja wa Ulaya ya kutetea sera za kubana matumizi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kuanguka serikali ya Uholanzi kunatishia kutetereka kwa mwasisi wa mchakato wa kuleta umoja wa Ulaya.

Hata hivyo mhariri anaeleza kuwa Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alifanya makosa kufikiri kwamba angelimvunja nguvu Wilders kwa kumwingiza katika serikali ya mseto. Wilders ambae ni mchukia uislamu, alijenga wingi katika serikali, lakini ilikuwa wazi kwamba siku moja angeliutumia wingi huo kuiangusha serikali. Na amefanya hivyo. Wilders ameiangusha serikali nchini Uholanzi bila ya kujali athari zake. Kwa hivyo mtu huyo hafai kuongoza nchi.

Mhariri wa "Süddeutsche Zeitung" anatilia maanani kwamba serikali ya Uholanzi imeanguka kutokana na sera za kubana matumizi.Mhariri huyo anaeleza kwamba sera ya kubana matumizi inayumba barani Ulaya. Anasema kuwa katika mwaka huu wa tano tokea mgogoro wa madeni uanze, hata zile serikali zilizoahidi kuitekeleza sera hiyo, sasa zinapiga chenga. Sababu ni maandamano ya kuipinga sera hiyo yanayofanywa na wananchi. Pia makampuni yanafilisika na kwa sababu serikali zinahofia kutimuliwa na wananchi. Mipango ya kubana matumizi yenye lengo la kuutatua mgogoro wa madeni na kuleta ustawi sasa imo katika hatari ya kusambaratika barani Ulaya.

Mhariri wa "Nordwest Zeitung" anasema ni vigumu kujua jinsi Uholanzi itakavyojiondoa kwenye mgogoro wake wa kisiasa kwani imesimama njia panda.

Mhariri wa gazeti hilo anasema, idadi ya wale wanaotetea sera za kubana matumizi ni ya wastani. Anaeleza kuwa wapinzani nchini Uholanzi ikiwa pamoja na Wilders, hawatachukua hatua ili kusaidia kuutatua mgogoro wa madeni. Mpango wa serikali wa hapo awali wa kupunguza malipo ya uzeeni ni baruti. Hali ngumu zitakuja barani Ulaya, ikiwa Uholanzi ,yaani mshirika mwenye uwezo mkubwa, itajitoa kwenye mfungamano wa wanaotetea sera za kubana matumizi.

Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linazungumzia juu ya mshikamano baina ya Kansela Merkel na Rais Nicolas Sarkozy baada ya kufanyika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa. Gazeti hilo linasema kuwa Kansela Merkel bado anaweza kutumia maneno mengi kumuunga mkono Sarkozy.

Lakini Merkel pia amesema atakuwa tayari kushirikiana na atakaeshinda uchaguzi nchini Ufaransa. Lakini ukweli ni kwamba nyota zimekaa kombo kwa urafiki wa Merkel na Sarkozy. Mambo pia siyo mazuri kwa bara la Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman